Ufanisi wa jeshi la Nigeria dhidi ya Boko Haram wajadiliwa

Wapiganaji 40 kati ya 57 wa Boko Haram waliojisalimisha huko Meri, Cameroon, Julai 29, 2021.(Moki Edwin Kindzeka/VOA)

Picha za wanamgambo wa Kiislamu wakiwa na nguo chafu pamoja na familia zao wakijisalimisha kwa jeshi la Nigeria zimezusha mjadala mkali juu ya madai ya jeshi la nchi hiyo la ufanisi katika vita vyake vya muda mrefu na mustakbali wa wapiganaji wanaoweka chini silaha zao.

Mamia ya wanachama wa kundi la Boko Haram wamekuwa wakionyeshwa kwenye picha na video za jeshi mwezi huu wakijisalimisha kwa wanajeshi katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno.

Baadhi ya wanachama wa Boko Haram wakiwa wamepewa mabango yaliyoandikwa kwa mkono kuwaomba wanigeria kuwasamehe.

Jeshi la Nigeria linaeleza kujisalimisha huko ni ushindi wa kampeni yake inayoimarika katika lengo la kumaliza vita vya karibu miaka 12 vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 na karibu milioni 2 kukoseshwa makazi yao.

Lakini wachambuzi na baadhi ya maafisa wa usalama wanasema kujisalimisha kwa wingi wapiganaji hao huenda kunatokana na kushindwa kwa Boko Haram hivi karibuni kutokana na ugomvi wao wa ndani na wapinzani wao wa kundi jingine la wanamgambo wa Kiislamu la Islamic State of West Africa Province, ISWAP.