Vurugu hiyo inabainisha kuwepo na hasira na mivutano ya juu ndani ya ukumbi wa taifa wa kuhesabu kura wakati nchi ikisubiri matokeo rasmi kutangazwa kutokana na upigaji kura wa Jumanne iliyopita. Kulikuwa na mashara yakiendelea mitandaoni kuhusu mivutano hiyo kutoka kwa raia ikielezea kuwa wengine wote katika taifa hilo wanaendelea kuwa na subira.
Katika kinyang’anyiro cha urais, matokeo hadi sasa yanaonyesha ushindani mkali kati ya kiongozi wa upinzani mwenye mrengo wa kushoto Raila Odinga na mfanyabiashara aliyejiendeleza mwenyewe Naibu Rais William Ruto.
Lakini mkanganyiko juu ya kujumuisha kura unaofanywa na vyombo vya habari na hatua ya polepole ya tume ya uchaguzi vimeongeza wasiwasi nchini Kenya, ambayo ni nchi tajiri zaidi na imara katika Afrika Mashariki, licha ya kuwa na historia ya ghasia baada ya chaguzi kadhaa zilizokuwa na utata.
Shirika la habari la Reuters halikuweza kuwapata maafisa wanaoendelea kujumuisha kura za uchaguzi wa rais Jumapili. Matangazo yaliyokuwa hewani yanayoonyesha matokeo katika kituo cha kujumuisha kura yalipotea saa kadhaa baadae.
Alipoulizwa kuhusu kujumuisha kura, msemaji wa tume aliwaelekeza Reuters kwenda kwenye matangazo yaliyokuwa hewani.
Matokeo rasmi yaliyothibitishwa Jumamosi yalikuwa ni juu kidogo ya zaidi ya asilimia 26 ya kura zilizohesabiwa yakionyesha Odinga alikuwa anaongoza kwa asilimia 54, huku Ruto akiwa na asilimia 45.
Mshindi ni lazima apate asilimia 50 na moja ya ziada. Tume hiyo ina siku saba tangu upigaji kura kuwatangaza washindi.
Majumuisho ya Shirika la habari la Reuters ya matokeo ya awali ya majimbo 255 kati ya 291 muda wa saa sita mchana kwa saa za Afrika Mashariki (0900 GMT) Jumapili yanaonyesha Ruto akiongoza kwa asilimia 52 na Odinga akiwa na asilimia 47. Wagombea wawili wengine walipata chini ya asilimia 1 ya kura kati yao.
Reuters haikujumuisha fomu 19 katika kuhesabu kwa sababu hazikuwa zimesainiwa, majumuisho hayasomeki vizuri au zilikuwa na matatizo mengine.
Majumuisho ya awali yanatokana na fomu kadhaa ambazo zinatakiwa kuthibitishwa iwapo kuna dosari zozote zitazogunduliwa wakati wa mchakato wa uthibitisho rasmi.
Hatua mbalimbali za kuhakiki na kuthibitisha matokeo zimewekwa ili kujaribu kuzuia tuhuma za wizi wa kura ambazo zilichochea ghasia mwaka 2007, huku zaidi ya watu 1,200 waliuawa na mwaka 2017, ambapo zaidi ya watu 100 waliuawa.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AP