Ubaguzi wa rangi dhidi ya Waafrika waripotiwa China

Baadhi ya Waafrika wakiwa katika mitaa ya jiji la Guangzhou katika jimbo la Guangdong. Picha na REUTERS/James Pomfret.

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, HRW, imegundua kwamba maudhui ya ubaguzi wa rangi yanayodhalilisha watu weusi yameongezeka nchini China.

Na kuwa jambo la kawaida kwenye internet na mitandao muhimu ya kijamii ya nchi hiyo, na maafisa wameshindwa kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo.

Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu limechunguza mamia ya video na maandishi yaliyochapishwa kwenye mitandao mashuhuri ya kijamii ya Uchina ikiwa ni pamoja na Bilibili, Douyin, na Xiaohongshu, tangu mwishoni mwa mwaka 2021.

Kulingana na ripoti, aina moja ya video ambayo imesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii ya kichina inawaonyesha waafrika ni watu maskini na wategemezi huku wachina ambao wengi wao ndio wanaotayarisha maudhui hayo wanaonekana kama matajiri, wanaotoa ajira, makazi na fedha.

Yaqui Wang mtafiti kutoka Human Rights Watch amesema kuenea kwa maudhui ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Waafrika kwenye mitandao ya kijamii ya nchi hiyo kumechochewa na serikali ya China inayoionyesha Afrika likiwa bara "maskini, lililo nyuma" ambalo linahitaji uwekezaji kutoka China.

"Tofauti na Marekani, ambapo ubaguzi wa rangi unajadiliwa sana katika vyombo vya habari na wasomi, China hakuna uhuru wa vyombo vya habari na taaluma , hivyo ni vigumu kwa maudhui mazuri yanayopinga ubaguzi kuenea," Wang aliiambia Sauti ya Amerika.

Hata hivyo ripoti hiyo, shirika hilo linasema sehemu kubwa ya maudhui hayo yanabuniwa ili kuzalisha fedha.