Your browser doesn’t support HTML5
Lissu aliyekuwa mbunge wa upinzani kupitia chama cha CHADEMA aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere mjini Dar es salaam Jumatatu mchana akitokea Brussels, Ubelgiji ambako alikuwa kwa ajili ya matibabu.
Maelfu ya wananchi wengi wakiwa wamevalia rangi za CHADEMA na kupeperusha bendera za chama hicho walijitokeza katika uwanja huo kumlaki kiongozi huyo ambaye tayari ameomba chama chake kimteue kugombania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba. Endapo atapata ridhaa ya chama chake atapambana na Rais John Magufuli ambaye ameteuliwa na chama tawala cha CCM kuwania muhula wa pili.
Lissu amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 2017 aliponusurika katika jaribio la kumwua baada ya kupigwa risasi kadha nje ya nyumba yake mjini Dodoma akiwa anatoka katika shughuli za bunge.
Baada ya shambulizi hilo Lissu alipelekwa Nairobi kwa upasuaji wa haraka na baada ya wiki kadhaa Nairobi alipelekwa Brussels, Ubelgiji ambako amekuwa akiendelea na matibabu.
Kutokana na matibabu hayo Lissu anasema mguu wake mmoja umekuwa mfupi na sasa anatembea kwa kuchechemea kidogo.
Chama cha CHADEMA hakijatoa ratiba kamili ya shughuli za Lissu baada ya kuwasili nchini humo. Wachambuzi wanadhani huenda chama hicho kitasubiri mpaka baada ya maziko ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Benjamini William Mkapa aliyefariki wiki iliyopita na anayetazamiwa kuzikwa Jumatano.