Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:46

Tundu Lissu: Nitarejea Tanzania Julai 27


Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa chama cha Chadema, Tanzania.
Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa chama cha Chadema, Tanzania.

Makamu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Chadema nchini Tanzania Tundu Lissu Jumanne alitangaza rasmi kurejea nyumbani Tanzania siku ya Jumatatu Julai 27 mwaka huu ili kushiriki shughuli za kisiasa nchini humo.

Akizungumza kwa njia ya mtandao wa Zoom, Lissu aliwashukuru Watanzania wanaoendelea kumtakia heri njema.

"Nawashukuru ndugu zangu Watanzania kwa kuniombea na kujitolea kuhakikisha ninatibiwa na kupona," alisema mwanasiasa huyo akiwa nchini Ubelgiji.

Haya yalijiri katika siku ambayo tume ya uchaguzi ya Tanzania ilitangaza kwamba uchaguzi mkuu utafanyika tarehe 28 mwezi Oktoba mwaka huu.

Tayari Lissu ametangaza kwamba atawania nafasi ya urais iwapo chama chake kitaridhia.

Kuhusu usalama wake, Lissu alisema wakati wale waliotenda uovu dhidi yake wanaitwa wasiojulikana, anaamini kwamba bado wapo na wana lengo hilo na kuna hatari katika maisha yake, akisisitiza kwamba hatari haijaondoka na kwamba mwenyekiti wa chama chake ameandika barua kuomba ulinzi kutoka katika vyombo vya usalama vya Tanzania lakini hajajibiwa.

Alisema hana ulinzi binafsi wa aina yoyote au kutoka nchi yeyote akiongeza kwamba wajibu wa kulindwa kwake ni kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, na kwa hivyo ni jukumu la jeshi la Polisi la nchi hiyo.

Kuhusu suala la kesi yake iliyoko katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, alisema ametishiwa sana kwamba akirejea atakamatwa, lakini akaongeza kwamba ana kesi 6 katika Mahakama ya kisutu ambazo zote ni kauli zake za kukosoa au kupinga sera za serikali ya Tanzania.

Lisu aklongeza kwa mujibu wa sheria za nchi, kwa ufahamu wake, yote aliyoshitakiwa nayo siyo makosa ya jinai na kwamba mahakama haijawahi kufuta dhamana yake akisema anarudi kama raia huru asiye na kosa lolote la jinai.

Aidha Lissu amesema anajua ana damu ya watanzania, wakenya na wabelgiji asiowafahamu baada ya kuwekewa damu katika matibabu yake hospitali za Dodoma, Nairobi na Ubelgiji alikofanyiwa upasuaji mara saba .

Pia amemshukuru mwenyekiti wa chama chake Freeman Mbowe na wanachama wa Chadema na vyama vingine nchini humo.

Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa sababu "ni muhimu kuliko wowote nchini humo."

Mwanasiasa huyo alipigwa risasi kadhaa mwaka 2017 na amekuwa akipokea matibabu nchini Ubelgiji baada ya kuhamishiwa huko kutoka hospitali moja nchini Kenya.

-Imetayarishwa na Sunday Shomari, VOA, Washington DC.

XS
SM
MD
LG