Trump, Johnson wakubaliana kupanua wigo wa biashara

Rais Donald Trump, kushoto, na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson walipokutana asubuhi katika Hoteli ya du Palais pembeni ya mkutano wa G-7 summit in Biarritz, France, Jumapili, Agosti, 25, 2019. (AP Photo/Andrew Harnik)

Rais Donald Trump na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson wamekubaliana kupanua wigo wa biashara kati ya nchi zao, Jumapili, kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano G7.

Trump na Johnson wamekutana kwa mara ya kwanza tangu Uingereza ipate Waziri Mkuu huyo mpya, na kuzungumzia kuongeza wigo wa biashara kati ya nchi zao baada ya Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya, Brexit.

Shirika la habari la AFP limeripoti mkutano huo na kuongeza kuwa viongozi kutoka nchi saba matajari zaidi duniani G7 wanaokutana mjini Biarritz, Ufaransa, hawatakuwa na taarifa ya pamoja mwaka huu wakati mkutano utakapomalizika.

Mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ameeleza lengo ni kuepusha mivutano itakayotokana na kutokubaliana.

Wanadiplomasia wanaeleza kuwa sio siri kuwa Marekani haikubaliani na Rais Macron na viongozi wengine juu ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Wakati huo huo maoni ya Rais Donald Trump juu ya biashara ya kimataifa na maamuzi yake ya kuzitoza ushuru zaidi bidhaa kutoka nchi washirika wa Marekani sawa na maadui zake yamesababisha sintofahamu.

Wachambuzi wa mambo ya kidiplomasia wanaeleza Boris Johnson ambaye anahudhuria mkutano kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani mwezi Julai 2019, kwa ahadi ya kuiondoa Ungereza Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, na kurudisha hadhi ya taifa lake, atakuwa anafuatiliwa zaidi katika duru za habari.

Mazungumzo kati ya Johnson na Rais wa Tume ya Ulaya Donald Tusk yatakayo fanyika Jumapili huenda yakawa na msuguano baada ya kuwepo mvutano Jumamosi juu ya nani wakulaumiwa iwapo Uingereza itaondoka Umoja wa Ulaya bila ya kufikia makubaliano.

Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa G7 kikao hicho kinatarajiwa kuangalia masuala ya uchumi wa kimataifa, biashara na usalama.

Baada ya chakula cha mchana, marais, mawaziri wakuu na viongozi wa mashirika ya kimataifa wanaohudhuria mkutano huo watajadili juu ya kukosekana usawa ulimwenguni. Washindi wa tuzo ya amani Nobel Denis Mukwege na Nadia Murad watazungumzia masuala ya usawa wa kijinsia katika kikao hicho cha G7.

Baadae viongozi kutoka bara la Afrika watahutubia. masuala yanayohusiana na eneo la Sahel yanayokabaliwa na wimbi la makundi ya kigaidi na yatapewa umuhimu maalum.