Trump huenda akatangaza mpango wa amani wakati utakapofanyika uchaguzi Israeli

Rais Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump amezungumzia masuala mengi akiwa katikati ya muhula wa uongozi wake akisema huenda akasubiri hadi uchaguzi mkuu wa Israeli, ndipo atakapotangaza mpango wa amani kwa kanda ya Mashariki ya Kati ambao umetayarishwa na mkwe wake Jared Kushner

Donald Trump alisema : "Pengine nitasubiri au nitatangaza sehemu ya mpango huo. Tuna watu wenye ustadi kama mnavyowafahamu balozi wetu na wengine. Lakini huenda huo ukawa mkataba mgumu kabisa kufikia amani kati ya Waisraeli na Wapalestina."

Wapalestina tayari wamepinga mpango unaopendekezwa na utawala wa Trump na walisusia mkutano wa Bahrain uliyotayarishwa na Kushner juu ya mpango wa uchumi kwa Palestina.

Akigeukia mazungumzo ya biashara na China alisema China inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi na imepoteza nafasi milioni mbili za ajira katika muda mfupi.

Trump ameeleza kuwa : "Wanapoteza karibu nafasi milioni mbili za ajira kama mnavyo fahamu kwani munaripoti juu ya hali ya mambo huko. wanataka tufikiye makubaliano. Tutaona kitakachotokea lakini bila shaka wanataka kufikia makubaliano."

Kuhusiana na maandamano ya Hong Kong ambayo yalifanyika kwa amani hapo Jumapili, Trump alifananisha hali hiyo na maandamano ya ghasia ya Beijing ya Uwanja wa Tianamen 1989.

Hong kong

Rais Trump aliongeza : "Ningelipenda kuona Hong Kong itatanzua matatizo yao kwa njia ya kibinadamu. Natumaini Rais Xi anaweza kufanya hivyo. Bila shaka ana uwezo huo. Ninadhani itakua jambo zuri kwa mazungumzo ya biashara yanayoendelea."

Vile vile alipongeza jinsi mazungumzo yanavyoendelea pamoja kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan, akisema mambo yanadhibitiwa vyema na yote inategemea msimamo wa serikali ya Afghanistan na Wataliban pia.

Akizungumzia juu ya Iran wakati meli ya mafuta iliyoshikiliwa Gilbrata ikondoka Jumapili usiku baada ya mvutano na nchi za Ulaya, Rais Trump alisema anadhani Tehran ingelipenda sana kuzungumza na Washington kufikia makubaliano lakini bado hawajui vipi waanze.

Jambo moja ni kwamba ni watu wa Iran ni wenye fahari sana. Lakini uchumi wao unaporomoka. Ninadhani Iran wanataka kufikia katika mazungumzo na wanauwezo mkubwa. Na ninataka kusema hivyo pia upande wa Korea Kaskazini.

Kuhusiana masuala ya ndani Trump alikiri kwamba alizungumzia suala la kuchukua umiliki wa Greenland kutoka Denmark, lakini alisema sio suala muhimu kwa hivi sasa. Na alisema Makamu Rais Mike Pence atakuwa tena mgombea mwenza atakapo tangaza anawania tena kiti cha urais 2020.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.