Trump atakiwa kufika mbele ya kamati ya bunge kutoa ushuhuda

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump.

Kamati ya bunge la Marekani inayochunguza matukio yaliyopelekea shambulizi la Januari 6, mwaka 2021, ilipiga kura kwa kauli moja Alhamisi, kumtaka Rais wa zamani Donald Trump, afike mbele yake kutoa ushuhuda wake binafsi.

Katika kikao kilichofanyika Alhamisi mjini Washington DC, video mpya inayotia wasiwasi, ya wasaidizi wake wa karibu, wakielezea mpango wake madhubuti, wa kutengua matokeo ya uchaguzi wa 2020 ilionyeshwa.

Wachambuzi wanasema matamshi ya Trump ndiyo yalipelekea wafuasi wake, kutekeleza shambulizi baya, dhidi ya bunge la Marekani.

Jumbe za kutisha kutoka kwa maafisa wa usalama, zikionya juu ya ghasia, na video mpya ya Spika wa Baraza la wawakilishi, Nancy Pelosi, na viongozi wengine wa bunge, wakiomba msaada, zilionyesha hali halisi siku hiyo, ambapo waliokuwa kwenye jengo la bunge, walikuwa karibu kukata tamaa.

Shirika la habari la AP linaripoti kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba Trump atapinga uamuzi huo wa kamati ya bunge.