Tanzania yakerwa na angalizo la usalama lililotolewa na ubalozi wa Marekani

Ramani ya Tanzania

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania imemuita Kaimu Balozi wa Marekani wizarani kutokana na angalizo la kiusalama lililotolewa na ubalozi huo juu ya uwezekano wa kuwepo shambulio katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Ubalozi ulitoa taarifa hiyo kupitia mtandao wa kijamii “Twitter” Jumatano.

Taarifa iliyotolewa na wizara imesema ilimwita Kaimu Balozi wa Marekani ili atoe ufafanuzi wa “twitter” hiyo na ubalozi huo ukamtuma mwakilishi wa Kaimu Balozi, Ann Marie Warmenhoven – Tilias kukutana na uongozi wa Wizara.

Wizara imedai kuwa mwakilishi huyo ameutambua ujumbe huo na kukiri kuwa ulitumwa na ubalozi wa Marekani.

Taarifa ya wizara imesema katika ufafanuzi wake mwakilishi amekiri kuwa Ubalozi ulifanya makosa kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote, wakitambua kuwa ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo, jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.

Wizara imesema imeukumbusha ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Faraji Kasidi Mnyepe amewataka wananchi na jumuiya za kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Amesema kuwa mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimejizatiti kukabiliana na vitisho vyovyote.