Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Nairobi, Kenya, Kanze Mararo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan atakuwa katika ziara nchini humo kwa siku mbili ambapo atapokelewa na mwenyeji wake Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Ziara ya Rais Samia itakuwa ya pili nje ya nchi tangu kuchukua madaraka baada ya kifo cha hayati John Pombe Magufuli. Kwanza alienda Uganda kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima mpaka Tanga.
“Rais Uhuru Kenyatta atampokea Rais Samia Hassan Suluhu, ikulu siku hiyo hiyo, Mei 4. Taarifa nyingine kuhusu ziara ya Rais Samia Hassan Suluhu zitaendelea kutolea,” amesema Mararo kwenye taarifa yake.
Alipotafutwa msemaji mkuu wa Serikali na mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa kuzungumzia kuhusu ziara hiyo alisema “Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa watalielezea hilo,” vimeeleza vyanzo vya habari Tanzania
Na alipotafutwa mkurugenzi wa habari wa Wizara ya Mambo ya Nje, Emmanuel Buhohela amesema “Waziri atalizungumzia hilo, nadhani kesho. Naomba usubiri kupata taarifa za kina kutoka kwake.”
Alipokuwa akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Taifa lake, jijini Dodoma wakati wa maombolezo ya Rais Magufuli, Rais Kenyatta alimkaribisha Rais Samia nchini Kenya.
Kama hiyo haitoshi, Aprili 10, Kenyatta alituma ujumbe maalumu nchini ulioongozwa na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi wa nchi hiyo, Balozi Amina Mohamed.
Taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema Rais Samia alizungumza na Balozi Amina wa Kenya alipozuru Tanzania mapema mwezi huu kuhusu dhamira ya Kenya kuendeleza na kukuza uhusiano na ushirikiano katika nyanja tofauti hususan kiuchumi na kijamii.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alimhakikishia Kenyatta kwamba Serikali ipo tayari kuendeleza mazuri yaliyoasisiwa na watangulizi wake na kutatua changamoto zilizopo kati ya mataifa haya mawili, wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kupitia ujumbe huo pia, Kenyatta alimwalika Samia kufanya ziara nchini Kenya ili kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano huku akiahidi kwamba Kenya ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania.