Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:43

Samia asema atakutana na wapinzani


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amelihutubia bunge la Tanzania kwa mara ya kwanza Alhamisi tangu achukue urais mwezi uliopita baada ya kifo cha mtangulizi wake John Magufuli.

Rais akizungumza katika Bunge mjini Dodoma, ametumia muda mrefu kuzungumzia mbinu mbali mbali za ukuzaji uchumi na pia kutangaza kuwa atakutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini humo kujadili mwelekeo mpya wa demokrasia baada ya miaka sita ya vyama vya upinzani kulalamika kuwa vinabanwa kidemokrasia.

“Naomba nilieleze Bunge hili tukufu pamoja na Watanzania kuwa dira na mwelekeo wa awamu ya sita itakuwa ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya. Kimsingi ndio dhana na maana halisi ya kauli mbiu au salamu yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi iendelee, tutaenzi na kuendeleza mambo yote mazuri lakini pia tutafanya mabadiliko pale itakapobidi kwa lengo la kukuza ufanisi na tija.

Uwajibikaji

“Hatutakuwa tayari kuvumilia uvivu, uzembe na ubadhirifu wa mali au fedha za umma na tutaboresha mazingira ya uwekezaji na kuvutia zaidi wawekezaji, wa ndani na nje ya nchi,” Rais amesema.

Uchumi wa Tanzania

Rais Samia amesema uchumi wa Tanzania ulipungua kutoka asilimia 6.9 hadi 4.7 hasa katika kipindi cha janga la virusi vya korona, na serikali yake itafanya juhudi kufufua uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato katika sekta za kilimo, viwanda na madini.

Janga la Korona

Hata hivyo, Rais Samia hakuwa na jipya kuhusu jinsi serikali yake itakavyopambana na janga la Korona isipokuwa kurudia kuwa ameunda tume ya wataalam itakayoishauri serikali jinsi ya kupambana na janga hilo. Lakini aliwataka Watanzania kuchukua tahadhari zinazotolewa na taasisi za ndani na za kimataifa katika kupambana na virusi hiyo.

Kuboresha Miundombinu

Rais Samia aliwaondoa wasiwasi watanzania kwa kusema kuwa serikali yake itaendeleza na kukamilisha juhudi zilizofanywa na serikali ya hayati John magufuli katika kuboresha miundo mbinu kama barabara na reli, pamoja na usafiri wa majini pia.

Vyombo vya utoaji haki

Rais Samia alisema pia atashirikiana na vyombo vya sheria kuhakikisha kuwa vinajielekeza zaidi katika kutenda na kutoa haki kwa wananchi. Lakini akakemea vikali utumiaji wa mitandao ya kijamii kuzusha hofu nchini humo.

Ukosoaji wa serikali

Rais Samia amewataka wabunge wasisite kuikosoa serikali yake pale wanapohisi kuna mambo ambayo hayaendi sawa na kuna haja ya kurekebishwa na kusema ukosoaji uwe mkali lakini itumike lugha ya kibunge na kuwaeleza mawaziri wake kuwa wakubali kukosolewa.

Mwanamke katika Uongozi

Rais Samia amelieleza bunge na watanzania kwa jumla kwamba wale wenye wasi wasi kuwa yeye ni ‘mwanamke atashindwa kutekeleza majukumu,’ hiyo dhana ambayo haina ukweli.

“Mwenyenzi mungu hakuumba ubongo hafifu kwa mwanamke na ubongo makini kwa mwanamme,” amesema na kuongeza kuwa amekuzwa katika jamii sahihi na ana uzeofu wa kutosha katika serikali na chama tawala cha CCM kuliongoza taifa la Tanzania.

Ushirikiano

Amesema atashirikiana na kila mmoja katika ngazi tofauti katika kuleta maendeleo ya uchumi, elimu, jamii, siasa na uchumi na kuwarai watanzania “tushikamane na tushirikiane kwa manufaa ya taifa la Tanzania.”

XS
SM
MD
LG