Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 05:22

Tanzania : Rais Samia afanya mabadiliko madogo Baraza la Mawaziri


Rais Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri muda mfupi baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania Ibrahim Hamis Juma kumuapisha Makamu wa Rais, Philip Mpango.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia Suluhu amebadili baadhi ya mawaziri na kuwapanga upya lakini akiwaacha wote kwenye baraza hilo.

Mabadiliko makubwa ameyafanya kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo amemteua balozi Liberata Mulamula kuwa mbunge na baadaye kumteua kushikilia wizara hiyo.

Waziri aliyekuwa akitumikia Wizara ya Mambo ya Nje Palamagamba Kabudi akirejeshwa kwenye Wizara ya Katiba na Sheria.

Waziri wa Fedha na Mipango amekuwa Mwigulu Nchemba.

Kadhalika mabadiliko mengine ameyafanya Ofisi ya Rais,TAMISEMI, ambapo amemuondoa Selemani Jafo na kumpeleka ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na nafasi yake kuchukuliwa na Ummy Mwalimu kama Waziri wa TAMISEMI.

Awali Rais Samia Suluhu alimzungumzia Makamu wa Rais Philip Mpango kwamba ni mtu muadilifu anaona ataweza kumsaidia kwenye masuala ya kiuchumi na udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali.

Baadhi ya wachumi jijini Dar es Salaam wakimzungumzia Makamu wa Rais Mpango pia wamesema wanaiona Tanzania katika mabadiliko zaidi kiuchumi kutokana na uzoefu wake katika usimamizi wa masuala ya fedha alipokuwa waziri wa fedha na mipango .

Katika hatua nyingine Rais Samia Suluhu pia amemteua balozi Hussein Katanga kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuchukua nafasi ya Dkt Bashiru Ali ambaye amemteua kuwa Mbunge.

XS
SM
MD
LG