Wakati nchi hiyo inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya mtoto, watumishi serikali na zile zisizo za kiserikali wametakiwa kuacha kukaa ofisini na kusubiri matatizo.
Akizungumza na Sauti ya Amerika Mwanaidi Kombo ambaye ni Mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) amezitupia lawama baadhi ya Taasisi zinazopambana na ukatili dhidi ya watoto kwa kuajiri wafanyakazi wasio na weledi ambao wamekuwa wakitoa taarifa za waathirika wa vitendo vya ukatili ambazo zilipaswa kuwa siri na hivyo kupelekea taharuki katika jamii.
“Tupeleke watu ambao ni weledi kuepuka hizi taharuki, lazima tujue tunapeleka watu wa namna gani katika suala zima la utoaji wa elimu, tunapeleka watu wa namna gani katika kuwahudumia hawa waathirika wa ukatili wa kijinsia” alisema Kombo
“Kwasababu sasa imekuwa ule usiri, haiba ya kuwahudumia hawa waathirika wa ukatili wa kijinsia sio nzuri kiasi ambacho kila mtu amekuwa ni msemaji kitu ambacho pengine kitakuja kuleta makovu” aliongeza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu inasema kwa mwaka 2022 pekee jumla ya watoto 12,163 walifanyiwa ukatili na kati ya hao 6,365 ilikuwa ni matukio ya ubakaji huku hali ikionekana kuzidi kuwa mbaya ikilinganishwa na miaka miwili nyuma ambapo kwa mwaka 2021/2022 jumla ya watoto 5,899 waliripotiwa kufanyiwa vitendo vya ubakaji.
Ili kupunguza ongezeko la vitendo vya ukatili Mwalimu Rehema James kutoka shule ya wasichana Bweranyange iliyopo Karagwe amesema Taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zinapaswa kutoa elimu kabla ya vitendo vya ukatili kujitokeza na kuachana na tabia ya kufanya utatuzi baada ya kuwa tayari vitendo hivyo vimekwishautokea.
“Baada ya taasisi kusaidia kutoa elimu wazazi wasiwazuie watoto kwenda shule wanakuja kuanzia pale watoto wamezuiwa kwenda shule ambapo wanawaokoa wachache sana wengi wanawapoteza kwahiyo hizi taasisi zikishuka zikaendelea kutoa elimu kwa bidii inavyopaswa kwasababu zipo kuanzia kwenye ngazi ya kata mafanikio ni makubwa tunakokwenda.” Alisema James.
Naye aliyekuwa mbunge wa Bunge la Tanzania ambae kwa sasa ni Naibu Katibu mkuu wa chama cha Wananchi (CUF) Magdarena Sakaya amesema serikali inapaswa kufanya ufuatiliaji wa taasisi zinazojishughulisha na watoto ili kubaini iwapo wanafanya kazi za utoaji elimu kwa usahihi kwakuwa watoto wengi bado wanapitia vitendo vya ukatili.
“Pia lazima serikali ihakikishe kwamba inapitia taasisi zote zinazoshughulika na masuala ya watoto, taasisi moja baada ya nyingine wapitei katiba zao na malengo yao waliyopanga kufanya nini na kuweze kuwepo na ufuatiliaji wa hizi taasisi ni kweli wanafanya kazi hizo au wanafanya kazi nyingine.” Alisema Sakaya.
Siku ya Watoto Duniani huadhimishwa kote duniani kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu haki, ustawi, na mahitaji ya watoto. Kauli mbiu ikiwa inasema "Kwa kila mtoto, kila haki" inaonyesha azma ya kuhakikisha kwamba kila mtoto ana haki zake zinazostahili na anapata fursa sawa katika maisha.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam