Afisa wa zamani wa al-Shabab, Omar Mohamed Abu Ayan aliiambia Sauti ya Amerika kuwa kamanda huyo mkongwe wa kijeshi Osman Mohamed Abdi, anayejulikana kama Moallim Osman, alikuwa mlengwa.
Jina la mlengwa na cheo chake pia vilithibitishwa na Wizara ya Habari ya Somalia katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne. Wizara hiyo ilisema Moallim Osman alikuwa akishughulikia upelekaji wapiganaji wa kigeni nchini Somalia ili kuisaidia al-Shabab.
Alionekana kunusurika katika shambulio la anga, msemaji wa Kamandi ya Marekani Afrika alisema.
"Kufuatia tathmini ya kina ya uharibifu wa vita, U.S.-AFRICOM imeonyesha kuwa kiongozi mmoja wa al-Shabab alijeruhiwa kutokana na operesheni hiyo," msemaji wa AFRICOM, Luteni Kamanda Timothy S. Pietrack, aliiambia Sauti ya Amerika siku ya Jumanne.
Shambulio hilo lilifanyika siku ya Jumamosi huko Jilib, ngome ya al-Shabab iliyoko takriban kilomita 385 kusini magharibi mwa Mogadishu.
"Tathmini ya awali ya kamandi ya kijeshi ni kwamba hakuna raia aliyejeruhiwa au kuuawa," taarifa ya AFRICOM ilisema.
Moallim Osman ni kamanda mkongwe ambaye ameshikilia nyadhifa kadhaa ndani ya kundi hilo la al-Shabab, ikiwa ni pamoja na kuwahi kuwa mkuu wa ulinzi, kulingana na afisa wa Somalia ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kutokuwa na mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Maafisa wa Somalia pia wanasema Moallim Osman alihusika katika kupanga mashambulizi yaliyofanywa na kundi hilo Januari 2016 dhidi ya kambi ya kijeshi ya Umoja wa Afrika inayosimamiwa na vikosi vya Kenya huko El Adde.
Ni shambulio baya sana kufanywa na wanamgambo hao dhidi ya walinda amani nchini Somalia na lilifanyika katika mji alikozaliwa Moallim Osman, kulingana na vyanzo vya usalama vya Somalia.