Wizara ya habari na mawasiliano kwenye ujumbe wa Twitter inaeleza kwamba lilikuwa onyo lisilo sahihi kuhusiana na mlipuko kwenye mlima Nyamulagira.
Wizara imeeleza kwamba picha zilizochukuliwa kwa ndege iliyo safiri kwenye eneo hilo la volcano zinaonyesha hakuna mlipuko wowote wa volcano na hakuna kitisho chechote kwa makazi ya maeneo ya kaskazini mwa mlima huo Jirani na ule wa Nyiragongo.
Taarifa ya wizara ya habari imeendelea kueleza kwamba moshi ulionekana na kusababisha kutolewa onyo ulitokana na kuchomwa kuni kwa ajili ya kupata mkaa, pamoja na wakulima kuchoma nyasi na kusababisha moshi mkubwa.
Mapema Jumamosi msemaji wa serikali alikuwa ametaja mlipuko kwenye mdomo wa volcano wa Murara kando ya volcano ya mlima Nyamuragira unaofahamika kua ni volcano yenye kutokota.
Watu wapatao 400,000 wameukimbia mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kufuatia onyo la kuripuka tena kwa volkano katika Mlima Nyiragongo.
Maafisa wa Goma wamesema familia 80,000 ambazo ni sawa na watu 400,000 waliondoka Goma Alhamisi kufuatia tahadhari iliyotolewa na serikali.
Wakati huohuo vyanzo vya habari vinaeleza serikali ya Congo inafanya jitihada za kutoa misaada ya maji ya kunywa, chakula na vifaa vingine na wafanyakazi wanasaidia kuwakutanisha watoto waliotengana na familia zao.
Awali, ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kiutu, OCHA, ilikadiria kuwa takriban watu 400,000 kati ya 600,000 wa mji huo wataathirika na agizo hilo ambalo limetolewa kwenye wilaya 10 kati ya 18.
Hadi sasa taarifa zinaeleza kuwa watu 34 wamekufa kutokana na athari za mripuko huo wa volkano wa juma lililopita.