Mashtaka hayo yamedai kwamba Menendez alifanya upendeleo kwa wafanyabiashara wa New Jersey badala ya malipo ya pesa taslimu na dhahabu.
Menendez atatokea kwa mara ya kwanza katika mahakama ya Manhattan kufuatia wito uliozidi kuongezeka kutoka kwa wafanyakazi wenzake ikiwemo wengine kutoka chama chake kwamba ajiuzulu.
Kesi yake inakuja siku moja baada ya mwanamme mmoja kushtakiwa kwa njama ya kumhonga Menendez na kufikishwa katika mahakama ya serikali kuu huko New York.
Wael Hana amekana mashtaka yake ikiwemo njama ya kufanya vitendo vya rushwa.
Hanna alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Kennedy huko New York jumanne baada ya kurejea kwa hiari kutoka Misri kukabiliana na mashitaka na kuachiliwa huru akisubiri kesi, aliamriwa kulipa dhamana ya dola laki tatu fedha taslimu na bondi ya dola milioni tano.