Rwanda, Uganda zafikia makubaliano kudumisha usalama

Rais Paul Kagame wa Rwanda (Kulia) na Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Wajumbe wa serikali za Rwanda na Uganda ambao wamekutana mjini Kigali Jumatatu, wamekubaliana mambo kadha ikiwemo kujiepusha na harakati za kuyumbisha usalama katika nchi mojawapo.

Katika taarifa ya pamoja iliyokamilisha kikao hicho, Rwanda imetoa orodha ya raia wake wanaozuiliwa nchini Uganda, na serikali ya Uganda imekubali kuchunguza kwa kina taarifa hiyo, na kuhakikisha wale ambao watakutwa hawana hatia kuachiliwa huru.

Pande hizo zimekubaliana pia kusahihisha mkataba wa kuwarudisha makwao watuhumiwa wa uhalifu. Wajumbe kwenye mkutano huo wa mjini Kigali wamekubaliana na kuachana na tabia ya kutumia vyombo vya habari au mitandao ya kijamii, kwa kufanya propaganda ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa nchi zao.

Aidha pande zote zimesema suala la uhuru wa usafiri wa watu na vitu kwenye mpaka wa nchi zao, litajadiliwa katika kikao kingine ambacho kitafanyika mjini Kampala, baada ya kipindi cha siku 30.

Ujumbe wa Uganda kwenye mkutano huo wa Kigali ulikuwa unaongozwa na waziri wa mambo ya nje, Sam Kutesa, nao ujumbe wa serikali ya Rwanda ulikuwa unaongozwa na waziri wa mashauri ya kigeni Olivier Nduhungirehe.

Waziri wa Mambo ya nje wa Angola Manuel Domingos Augusto, na naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, pia Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama Gilbert Kankonde Malamba, walishiriki kwenye mkutano huo kama wawakilishi wa wasuluhishi ambao ni marais wa Angola na DRC.

Walipokutana mjini Luanda, Angola, mwezi uliopita, marais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda walikubaliana kumaliza mzozo wa kisiasa kati ya nchi zao kupitia mazungumzo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.