Jeshi la anga la Ukraine lilisema mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo ilitungua droni zote nane zilizotumwa na Russia, lakini zilitungua makombora ya masafa marefu ya Russia 18 kati ya 51 yaliyoshambulia usiku kucha.
Jeshi la anga la Ukraine lilisema malengo hayo yaliyoshambuliwa na makombora ni pamoja na “miundombinu muhimu” na pia maeneo ya viwanda vya kijeshi na kiraia. Pia ilieleza kuwa siyo makombora yote yaliyokuwa hayajatunguliwa yaliweza kufikia malengo yake.
Oleksiy Kuleba, naibu mkuu wa ofisi ya urais ya Ukraine, alisema makombora ya Russia yalipiga eneo la maduka na majengo ya ghorofa huko Kryvyi Rih, mji wa kusini-kati ambao ni mji alikozaliwa Rais Volodymyr Zelenskyy. Kuleba alisema mtu mmoja aliuwawa.
Katika mkoa wa magharibi wa Khmelnytskyi, maafisa walisema kombora la Russia liliuwa mtu mmoja.
Oleg Synegubov, gavana wa kanda wa mkoa wa Kharkiv mashariki mwa Ukraine, alisema mtu mmoja aliuawa katika mji wa Zmiiv.
Mashambulizi hayo ya hivi karibuni yamekuja wakati Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg akiandaa kufanya mkutano wa Baraza la NATO na Ukraine Jumatano kujadili mashambulizi ya hivi karibuni yanayofanywa na Russia kwa kutumia droni na makombora, ambayo yamehusisha idadi kubwa ya droni na makombora ikilinganishwa na vita ilipoanza.
Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.