Hotuba kama hiyo aliitoa mwaka 2018 siku chache tu baada ya rais wa zamani Jacob Zuma kulazimishwa kuondoka madarakani kwa sababu ya kashfa za rushwa na Ramaphosa akashika hatamu za uongozi.
Katika hotuba yake ya takriban saa mbili ya hali ya taifa alizungumzia mambo mengi, kuanzia uchumi mpaka viwango vya ukosefu wa ajira ambavyo katika siku za karibuni vimepanda hadi asilimia 27.
Ramaphosa mfanyabiashara na mwanasiasa wa siku nyingi hakupata taabu kuainisha kipaumbele chake katika hotuba hiyo akielezea jinsi ya kuufufua uchumi wa nchi kwa manufaa ya raia wote.
“Juu ya yote hayo, lazima tuufufue tena uchumi wetu. Namtaka kila mwananchi wa Afrika Kusini kulipata kipaumbele suala hili. kwa sababu tumefanikiwa na kama tukifanya hivyo, kwa kweli, kama tutafanya hivi itakuwa kwa manufaa ya nchi nzima.
Hivi sasa,kama serikali, kama biashara, ajira, na raia wetu wote, lazima tuungane pamoja kuikumbatia kesho,” amesema rais Ramaphosa.
Ramaphosa aliingia madarakani kabla siku ya kutoa hotuba ya kuhusu hali ya taifa mwaka jana, baada ya rais wa zamani Jacob Zuma kupoteza umaarufu na kulazimishwa kuondoka mamlakani kutokana na kashfa kadhaa za rushwa.
Zuma hakuwa miongoni mwa marais wa zamani ambao walihudhuria hotuba ya Alhamisi usiku huko Cape Town.
Rais aligusia mambo mengi ambayo yanaikabili Afrika Kusini; lengo lake ni kuunga mkono na kuimarisha uchunguzi unaoendelea kuhusu rushwa shutma zinazomkabili Zuma na maafisa wengine wa juu; kampuni ya nishati amesema ataigawa katika sekta tatu; mabadiliko katika elimu, huduma za afya na nyumba za umma; jambo ambalo limekuwa ni jambo lake kuu la rais, na kufanya uamuzi wa kuteua kamati zaidi kuangalia masuala yenye umuhimu kwa taifa.