Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 17:16

Hatimaye Rais Jacob Zuma ajiuzulu


Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akitangaza kujiuzulu kwake kupitia hotuba ya moja kwa moja iliyorushwa na vituo vya televisheni.
Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akitangaza kujiuzulu kwake kupitia hotuba ya moja kwa moja iliyorushwa na vituo vya televisheni.

Jacob Zuma, aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, alitangaza kujiuzulu kwake Jumatano usiku alipolihutubia taifa katika matangazo yaliyopeperushwa moja kwa moja na vyombo vya habari nchini humo.

Katika hotuba yake, Zuma alisema kuwa hangependa kuona umwagikaji wa damu wala chama cha ANC kugawanyika kwa sababu yake.

"Nimewatumikia wananchi wa Afrika Kusini kadri ya uwezo wangu na ninawashukuru kwa kunipa nafasi hiyo," alisema Zuma kwenye hotuba yake ya dakika 30.

"Lakini nimechukua uamuzi wa kuachia madaraka mara moja," aliongeza.

Zuma, mwenye umri wa miaka 75 amekuwa akikabiliwa na kashfa kadhaa za rushwa na shinikizo kadhaa za kumtaka aachie mamlaka.

Mwansiasa huyo alisema kuwa ataendelea kulitumikia taifa na chama cha ANC licha ya kung'atuka madarakani.

Malumbano kati ya Zuma na chama cha ANC yalipelekea kuondolewa kwake kutoka kwa uongozi wa chama hicho na nafasi yake kuchukuliwa na makamu wake wa rais, Ceril Ramaphosa mwezi Desemba mwaka wa 2017.

Zuma ameiongoza nchi hiyo tangu mwaka wa 2009, kufuatia kujiuzulu kwa Rais Thabo Mbeki, ambaye pia alikabiliwa na tuhuma mbali mbali.

Mapema Jumatano, chama tawala cha ANC kilikuwa kimesema kuwa bunge lingepiga kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Rais Jacob Zuma Alhamisi, iwapo kiongozi huyo anayekabiliwa na tuhuma hangekubali kuachia madaraka mara moja.

Wanachama wa African National Congress (ANC) waandamana kumtaka Zuma kujiuzulu.
Wanachama wa African National Congress (ANC) waandamana kumtaka Zuma kujiuzulu.

Paul Mashatile, mweka hazina mkuu wa chama tawala cha ANC, ametangaza mpango huo Jumatano, siku ambayo Zuma alikuwa anatarajiwa kubainisha iwapo atakubaliana na matakwa ya chama chake kwamba aachie madaraka.

“Hatuwezi kuendelea kuachia Afrika Kusini isubiri bila ya majibu,” Mashatile amewaambia waandishi wa habari baada ya ofisi ya Zuma kukanusha taarifa zilizoenea kuwa walikuwa wamepanga muda wa Zuma kutoa tamko.

Viongozi wa ANC waliamua mapema wiki hii kusitisha uongozi wa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 75 baada ya kushikilia madaraka kwa miaka 9 ambao umegubikwa na tuhuma mbali mbali za ufisadi na kutokua kwa uchumi.

Madai hayo ni pamoja na tuhuma za kuwa Zuma ametumia kiasi cha dola milioni 20 za fedha za umma kwa ajili ya kuboresha nyumba zake binafsi.

Zuma alikuwa amekataa shinikizo kubwa la kujiuzulu la zaidi ya wiki moja kufuatia mazungumzo yaliyofanyika katika chama.

Kufuatia kujiuzulu kwake, rais wa ANC Cyril Ramaphosa anatarajiwa kuchukua usukani hadi uchaguzi utakapofanyika.

XS
SM
MD
LG