Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:55

Winnie Mandela afariki dunia


Winnie Mandela
Winnie Mandela

Mke wa Zamani wa Nelson Mandela, Winnie ambaye alishiriki katika harakati za kuutokomeza ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini amefariki akiwa na umri wa miaka 81. Taarifa hizi zimethibitishwa na msaidizi wake Winnie.

Kikundi cha watu wapatao 200 walifika nje ya makazi ya Winnie mara baada ya kifo chake wakiimba na kucheza. Pia baadhi ya viongozi wa taifa na wanasiasa walifika nyumbani kwake na polisi wakaufunga mtaa mzima.

Rais Cyril Ramaphosa alikuwa wa kwanza kati ya wale walioanza kutuma rambirambi wakiomboleza kifo cha Winnie nchini Afrika Kusini..

“Hivi leo tumempoteza mama, bibi, rafiki na komredi, kiongozi na fahari ya taifa," Ramaphosa alisema hayo katika hotuba yake iliyotangazwa katika televisheni kabla ya kufika nyumbani kwa marehemu Jumatatu jioni.

Kiongozi mstaafu wa kidini Afrika Kusini na mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi Askofu Desmond Tutu amesema: “ Ushujaa wake wa kupinga ubaguzi ulinihamasisha mimi, na kuhamasisha vizazi vilivyokuja vya wanaharakati.”

Waziri wa Nishati Jeff Radebe aliwasilisha rambirambi za chama cha ANC na kuwahimiza wale waliompenda Winnie kumuenzi.

Winnie alizaliwa Oktoba 26, 1936. Pamoja na kuwa Winnie na mumewe walitalikiana mwaka 1990, Winnie aliendelea kushiriki kuchangia maisha ya Mandela na aliendelea kuongoza harakati za siasa nchini Afrika Kusini.

"Kamwe sitakata tamaa na watu wangu hawatapoteza matumaini kamwe, bila shaka tunatarajia kwamba kazi itaendelea," alisema katika moja ya hotuba zake wakati akishiriki katika harakati hizo.

Wakati Mandela akitoka gerezani Winnie alikuwa yupo katika tukio hilo na walishikana mikono. Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27.

Winnie alianza kushiriki katika siasa wakati akiwa na umri wa miaka 20 na kuonyesha ujasiri mkubwa baada ya mumewe kuhumiwa kifungo cha maisha mwaka 1964 na serikali ya makaburu waliowachache nchini Afrika Kusini.

Kwa upande wa taaluma alijikita katika masomo ya huduma ya jamii na alipata umaarufu mkubwa katika nyanja za siasa na jamii.

.

XS
SM
MD
LG