Rais Samia awataka mawaziri wapya kufuata maadili ya kazi walizopewa

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri ambao anawateua kutekeleza majukumu yao ipasavyo wakizingatia mambo makubwa matatu -- kuheshimu katiba ya nchi, kufahamu mipaka yao na kutunza siri za Serikali.

Kufuatia uteuzi huu wananchi na wachambuzi wa kisiasa wamekuwa na maoni mchanganyiko juu ya mabadiliko hayo.

Rais Samia ametoa wito huo Jumatatu asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwaapisha mawaziri watatu aliyowateua Jumapii usiku.

Mara baada ya kuwaapisha Rais Samia amewataka viongozi hao kusimama imara katika kutekeleza wajibu wao na kuwa mstari wa mbele katika kuyasimamia majukumu ambayo wameapa kuyatumikia kwa moyo mkunjufu

Tangu Rais Samia alipochukua uongozi wa urais wa Tanzania baada ya kifo cha mtangulizi wake hayati John Magufuli hii ni mara ya tatu anafanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri huku wananchi wakiyapokea mabadiliko hayo kwa maoni tofauti.

Ismail Masudi Mkazi wa Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Sauti ya Amerika amesema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia yamekuja wakati muafaka huku akiongeza kuwa katika baadhi ya wizara zilizobadilishwa kulikuwa na mapungufu ambayo yalitakiwa kuzibwa mapema kabla ya mambo kuharibika siku za usoni.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wameonyesha kufurahishwa na mabadiliko hayo huku wakionekana kujawa na matumaini na viongozi wapya walioteuliwa lakini bado kwa wananchi wengine wanaona mabadiliko yanayofanywa hayatoshi kuleta utendaji kazi ulio bora ikiwa misingi na miiko ya uongozi haitaonekana.

Nassoro Kitunda ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mhadhiri msaidizi wa Chuo kikuu cha Kikatoliki Mwenge kilichopo Moshi amesema jambo muhimu kwa Serikali ya Tanzania ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa kumsaidia Rais wanatekeleza vyema majukumu yao kwa kufuata sera za nchi zinavyotaka, hivyo jambo la kubadili viongozi kila mara haliwezi kuwa ni jema kwa Taifa kama wateule hawatakuwa tayari kusimamia yale yanayohitajiwa na Nchi.

Rais Samia amewaapisha mawaziri watatu akiwemo Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Angellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Dkt. Stergomena Tax kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania