Daktari raia wa Tanzania anayefanya kazi nchini Uganda aliyeambukizwa Ebola amefariki dunia, mhudumu wa kwanza wa afya aliyefariki kwa ugonjwa huo katika mlipuko wa hivi karibuni nchini humo, waziri wa afya wa Uganda amesema Jumamosi.
"Nasikitika kutangaza kwamba tumempoteza daktari wetu wa kwanza, Dk. Mohammed Ali, raia wa Tanzania, Mwanaume mwenye umri wa miaka 37" Waziri wa Afya Jane Ruth Aceng, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Alisema Ali alifanyiwa vipimo vya Ebola Septemba 26 na kufariki wakati akipokea matibabu katika hospitali moja ya Fort Portal, mji ulioko umbali wa kilomita 300 magharibi mwa mji mkuu Kampala.
Mamlaka katika taifa hilo la Afrika Mashariki ilitangaza kuzuka kwa homa kali ya virusi vya Ebola Septemba 20 na kusababisha hofu ya mgogoro mkubwa wa kiafya katika nchi hiyo yenye watu milioni 45.
Hakuna chanjo ya Ebola yenye vimelea aina ya Sudan ambapo maambukizi yake yamezuka hivi karibuni nchini Uganda.
Wizara ya afya ilisema Ijumaa, kabla ya kifo cha Dr. Ali, kwamba ugonjwa huo hadi sasa umewaambukiza watu 35 na kuua watu saba.