Mswada huo wa IEBC ulikuwa mojawapo ya masuala yaliyotawala mjadala wakati wa maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali ya Kenya huku vijana wakitaka tume ya uchaguzi iundwe.
Kusaini kwa mswada huo sasa unatoa nafasi rasmi ya uteuzi wa jopo la litakalopendekeza makamishna wapya wa tume ya uchaguzi IEBC.
Akizungumza baada ya kutia Saini Mswada huo, Rais William Ruto alilitaka Bunge kuharakisha mchakato huo
“Naungana na viongozi ambao wamesema lazima kuwe na uwazi na uadilifu kama sehemu ya kanuni kuu za wanaume na wanawake watakaopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi wetu,” amesema rais Ruto
Kwa upande wake Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amesema changamoto mpya iliyopo kwa sasa inayochochewa na matakwa ya vijana wa kizazi kipya pamoja na raia kwa ujumla, inahitaji viongozi kutoa mwelekeo wa jinsi Kenya inapaswa kusonga mbele.
Odinga amesema “Ukiona masuala ambayo yametajwa na vijana wetu. Mengi yapo kwenye ripoti ya NADCO. Lakini kama ripoti hiyo itatekelezwa vizuri na kikamilifu, tunaweza kushughulikia masuala yote ambayo vijana hawa waliibua”
Operesheni muhimu za IEBC zilisimama kufuatia kumalizika kwa mhula wa tume iliyopita
Utaratibu wa kuteua Mwenyekiti na wajumbe wa tume unahusisha kuanzisha jopo la uteuzi angalau miezi sita kabla ya kumaliza muda wao au ndani ya siku 14 baada ya kutangazwa kwa nafasi wazi katika afisi hizo.