Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Januari 05, 2025 Local time: 09:54

Madaktari Kenya waweka kambi wizara ya afya


Madaktari Kenya wakiandamana kuelekea makao makuu ya Wizara ya Afya Aprili 9, 2024. Picha na SIMON MAINA / AFP)
Madaktari Kenya wakiandamana kuelekea makao makuu ya Wizara ya Afya Aprili 9, 2024. Picha na SIMON MAINA / AFP)

Madaktari nchini Kenya Jumatatu wamefanya maandamano jijini Nairobi na kuweka kambi katika Wizara ya Afya ili kuishinikiza serikali kuwaajiri madaktari wanafunzi katika vituo vya afya na kuwalipa mshahara kwa mujibu wa mkataba wa pamoja wa maafikiano wa mwaka 2017.

Mwezi Mei, baada ya siku 56 za mahangaiko makubwa katika hospitali za umma nchini humo, kufuatia mgomo wa madaktari, pande mbili kwenye mazungumzo hayo zilieleza kuwa zimefikia muafaka uliowezesha kutiwa saini mkataba wa kurejea kazini mara moja kama njia ya kipekee ya serikali kujitolea kutimiza utekelezaji kamili wa mkataba huo wa pamoja wa maafikiano wa mwaka 2017.

Mkataba ambao unaojumuisha masuala mbalimbali yakiwemo uajiri na ulipaji wa mshahara wa kila mwezi kwa madaktari wanafunzi, upanuzi wa mikataba ya wafanyakazi chini ya mfumo wa afya kwa wote, malipo ya ada kwa madaktari kwenye mafunzo ya uzamili, malipo ya malimbikizo ya mishahara ya kimsingi kulingana na CBA ya 2017 na; Utoaji wa Bima ya matibabu ya kina kwa madaktari.

Lakini baada ya kukamilika kwa kipindi cha miezi miwili kilichohitajika kukamilisha na kutatua masuala yanayofungamana na uajiri wa madaktari wanafunzi kwenye vituo vya afya na ulipaji wa mishahara, bado serikali haijaridhia hilo.

Dkt Davji Atellah, Katibu mkuu wa Muungano wa chama cha madaktari nchini humo KMPDU.aliiambia Sauti ya Amerika kuwa serikali ilihitaji kutimiza wajibu wake na iwapo haitatekeleza madaktari watalazimika kususia kazi kama shinikizo kwa serikali.

Muungano huo wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno KMPDU unawakilisha zaidi ya madaktari 7,000 nchini Kenya na unaeleza kuwa serikali haiwezi kujikokota au kushindwa kutekeleza kamilifu wa mkataba wa pamoja wa maafikiano wa mwaka 2017.

Ingawa serikali na madaktari hao waliafikia kutia saini mkataba wa kurejea kazini mara moja, walishindwa kufikia muafaka kuhusu mshahara wa kila mwezi wa madaktari wanafunzi wa shilingi elfu 206,000, ambao serikali iligomea ikisisitiza tu kuwa inaweza kuwalipa kitita cha shilingi elfu 70,000 kama mshahara wa kila mwezi na kisha kutoa ahadi ya kuwapa ajira, baada ya kipindi cha mwaka mmoja wanapohitimisha masomo ya nyanjani.

Waziri wa Afya Susan Wafula Nakhumicha, wakati huo alitangaza kuwa serikali italipa malimbikizo ya msingi ya mishahara, ufadhili wa masomo ya shahada ya kwanza, na bima ya matibabu na vile vile kukubali kuwasilisha shilingi bilioni 6.1 kutatua masuala 18 kati ya 19 yalioibuliwa na madaktari kwenye mgomo huo.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi.

Forum

XS
SM
MD
LG