Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 21:13

Maandamano Kenya: Wanasiasa, NGO, wafanyabiashara wanachunguzwa


Gari la polisi likichomeka nje ya bunge la Kenya wakati wa maandamano June 25 2024 AFP
Gari la polisi likichomeka nje ya bunge la Kenya wakati wa maandamano June 25 2024 AFP

Baraza la mawaziri la Kenya limesisitiza kwamba ni lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu waliojiingiza katika maandamano na kufanya uharibifu wa mali ikiwemo kuchoma majengo, wizi wa kimabavu miongoni mwa mengine.

Baraza hilo vile vile limewapongeza maafisa wa usalama walioshika doria wakati wa maandamano, na kuwataka maafisa waliotumia nguvu kupita kiasi kuchukuliwa hatua kulingana na kanuni za kisheria zilizowekwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari baada ya kikao cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na rais Dr. William Ruto, inasema kwamba maandamano ya kupinga mswada wa fedha 2024, yalianza kwa amani lakini yakaingiliwa na wahuni walioiba madukani, kuchoma magari, nyumba, biashara na kupelekea vifo.

Wanasiasa pia wanatajwa kuchochea ghasia wakati wa maandamano hayo na kwamba wote waliohusika na uharibifu lazima waadhibiwe.

Maafisa wa usalama wamesifiwa kwa kukabiliana na waandamanaji na kwamba walitenda kazi yao kulingana na maadili ya kazi licha ya mazingira magumu, na kwamba iwapo kuna afisa yeyote wa usalama aliyevunja sheria, anastahidi kuadhibiwa kulingana na kanuni zilizowekwa.

Ruto, ameliambia baraza lake la mawaziri kwamba wizara ya fedha inapanga upya bajeti kulingana na hali halisi ilivyo na matumizi ya pesa yatapunguzwa vilivyo na kwamba kuna miradi itakayositishwa bila ya kuvuruga mipangilio ya mipango muhimu ya serikali.

Ruto, amenukuliwa akisema kwamba mpango wake ni mzuri na haujatangishwa na kwamba ni muda tu ataondolewa lawama.

Hakuna idadi kamili ya kuaminika ya watu waliofariki kutokana na maandamano nchini Kenya. Wanaharakati wanasema watu 39 waliuawa, tume ya haki za kibinadamu inayofadhiliwa na serikali ikisema watu 22 pekee ndio waliofariki.

Wanaharakati walioitisha maandamano wamesitisha maandamano hayo wakisema kwamba yameingiliwa na wahuni waliokodishwa na wanasiasa kwa malengo yao binafsi.

Maafisa wa ujasusi wamechapisha picha za washukiwa wa ghasia na wengine kadhaa wamekamatwa.

Waziri wa ulinzi Aden Duale aliiambia runinga ya Citizen kwamba wanasiasa kadhaa, mashirika mawili yasiyo ya kiserikali, mfanyabiashara maarufu ni miongozi mwa watu wanaochunguzwa na polisi kwa kupanga maandamano na kwamba majina yao yatawekwa wazi hivi karibuni.

Forum

XS
SM
MD
LG