Ruto amesema serikali yake itapunguza matumizi kwa shilingi bilioni 177 katika mwaka huu wa fedha, huku fedha za ziada zinazohitajika, zikitoka kwa mikopo.
Haya yanajiri huku taarifa zikiibuka kwamba rais huyo alizungumza kwa njia ya simu na mkuu wa shirika la fedha Duniani, IMF, Kristalina Georgieva siku chache baada ya kukataa kutia Saini mswada wa fedha wa nchi hiyo, wa mwaka wa 2024, uliopendekeza hatua za kuongeza kodi, lakini ambao uliibua maandamano yaliyopeleka vifo, vyanzo viwili vya kidiplomasia vililiambia shirika la Habari la Reuters.
Mswada huo ulikuwa na umuhimu katika makubaliano ya mageuzi ya kisera, yaliyofikiwa kati ya Kenya na IMF, kama sehemu ya mpango wa kutoa mkopo wa dola bilioni 3.6 kwa taifa hilo.
Wachambuzi wanasema kutupiliwa mbali kwa mswada huo, huenda kukaathiri programu muhimu za maendeleo, hata ingawa serikali ya Kenya haihitaji fedha kwa dharura, kutoka kwa IMF, kwa sababu ilifanikiwa kulipa mkopo wa dola bilioni mbili, baada ya kuchukua mkopo mwingine wenye riba nafuu na ambao ungelipwa ndani ya kipindi cha miaka saba.
IMF imeshutumiwa na vijana wengi walioshiriki maandamano, wakiliona shirika hilo kama lililoshinikiza serikali ya Kenya kuongeza kodi.
Forum