Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 02:58

Kenya na Umoja wa Ulaya kuanza kutekeleza makubaliano ya biashara huru


Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen wakiwaangalia wawakilishi wakitia saini mkataba pya wa kiuchumi Nairobi on Desemba 18, 2023. Picha na LUIS TATO / AFP.
Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen wakiwaangalia wawakilishi wakitia saini mkataba pya wa kiuchumi Nairobi on Desemba 18, 2023. Picha na LUIS TATO / AFP.

Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda Bi. Rebeca Miano alitangaza Jumatatu kwamba Kenya na EU zimeanza kutekeleza Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) unaoruhusu kuingia kwa bidhaa za kila upande katika masoko yao bila ya kutozwa ushuru.

Ushirikiano huo ambao pia utaiwezesha Kenya kupanua mauzo yake ya nje kwenye soko la Ulaya, kuongeza mtiririko wa uwekezaji, na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi kwa matarajio ya kuzalisha ajira kwa raia wa Kenya.

Utekelezaji huo unafuatia kuweka saini mkataba huo kati ya rais wa Kenya William Ruto na rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, Desemba mwaka jana, jijini Nairobi, na kuweka wazi hatua za utekelezaji kamilifu.

Serikali ya Kenya inasema kuwa mkataba huo unaongeza kasi ya biashara, nafasi ya kusafirisha bidhaa za Kenya kwenye soko la nchi za Umoja wa Ulaya, lenye thamani ya dola trilioni 18 za Kimarekani, bila kutozwa ushuru wa forodha wala kuwekewa ukomo wa kiasi cha kuuza au kuwekewa tozo ndogo za ushuru wa forodha.

Umoja wa Ulaya ni kituo cha kwanza cha mauzo ya nje cha Kenya na mshirika wa pili wa kibiashara kwa ukubwa baada ya Benki ya Dunia. Ni fursa katika mojawapo ya masoko makubwa ya nje ya Kenya ambayo inachangia asilimia 21.1 ya jumla ya mauzo ya nje ya nchi ya Kenya, yenye thamani ya dola bilioni 1.4 za Kimarekani. Kwa sasa wanachama 27 wa EU wanachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na mauzo yake katika soko la Kenya kwa sasa yanafikia dola bilioni 2.1 za Kimarekani.

Rais Ruto wa Kenya na rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen wakipeana mikono baada ya utiajia saini wa makubaliano Desemba 18, 2023.
Rais Ruto wa Kenya na rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen wakipeana mikono baada ya utiajia saini wa makubaliano Desemba 18, 2023.

Charles Karisa ambaye ni mtaalam wa biashara, uchumi na uwekezaji nchini Kenya, anaeleza kuwa sasa ni bidii ya Kenya kuhakikisha inaongeza ujazo wa bidhaa zake kwenye soko la Ulaya kuongeza ujasiriamali na uwekezaji unaotabirika kujiendeleza.

Alisema kuwa Kenya inastahili kutumia mkataba huo kuimarisha ushindani wa soko lake la mauzo ya nje na kuacha mategemeo ya chai, kahawa, maua, nguo na chuma ambazo ndizo bidhaa zake muhimu kwenye soko la nje.

Mauzo ya kiasi kikubwa ya Kenya kwa soko la Umoja wa Ulaya ni bidhaa za kilimo kama vile mboga, matunda, chai na kahawa. Zaidi ya asilimia 70 ya maua yaliyokatwa nchini Kenya yanapelekwa kwenye soko la Ulaya.

Kupitia mkataba huu, wakulima wa Kenya wataongeza uwezo wa kipato na kupata uendelevu wa upanuzi wa soko linalotabirika hasa kwa samaki, mboga, matunda, maua, chai na kahawa. Aidha, mkataba huu unahimiza sekta binafsi za Umoja wa Ulaya kuwekeza nchini Kenya na kuchochea uzalishaji wa ajira katika sekta mbalimbali.

Mfanyakazi wa kiwanda cha kuhifadhia mimea huko Naivasha akisukuma mkokoteni uliojaa maua ya waridi yaliyokuwa yakisafirishwa kwa ajili kuuzwa katika soko la Ulaya.
Mfanyakazi wa kiwanda cha kuhifadhia mimea huko Naivasha akisukuma mkokoteni uliojaa maua ya waridi yaliyokuwa yakisafirishwa kwa ajili kuuzwa katika soko la Ulaya.

Mkataba huo unailazimisha Kenya kuunga mkono malengo ya kimataifa ikiwa ni dhamira ya kukuza demokrasia na utawala wa kisheria, kuheshimu haki za binadamu, kuwa sehemu ya jitihada za ulimwengu za kudumisha amani na usalama na vile vile kuunga juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, yakiwa ni masharti ambayo Kenya lazima iyatimize kuendelea kunufaika na mkataba huu.

Mkataba huu, vile vile, unalenga kutekeleza masharti ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ingawa ni mkataba wa kwanza wa kibiashara na maendeleo ya kiuchumu ambao Umoja wa Ulaya umeingia na nchi zinazoendelea, Umoja wa Ulaya unauona kama mlango wa wazi kuingia barani Afrika, kuwa mshirika mpya wa uwekezaji na kujenga maslahi yake ya kudumu, na unatarajiwa kuwa kielelezo kwa nchi nyingine za Afrika, hasa zile za Afrika Mashariki zinazohiari kuingia makubaliano hayo.

Mkataba huu ni kilele cha mazungumzo ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyoanza miaka saba iliyopita. Mwaka 2014, licha ya Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi na Rwanda kukamilisha mazungumzo ya makubaliano haya ya kiuchumi, ni Kenya pekee iliyosonga mbele kwa kasi na kuyaidhinisha kikamilifu.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi.

Forum

XS
SM
MD
LG