Rais Macron apanga upya utawala wake wakati serikali imejiuzulu

Rais Emmanuel Macron

Waziri Mkuu wa Ufaransa Edouard Philippe na serikali yake wamejiuzulu Ijumaa wakati Rais Emannuel Macron akichukuwa hatua ya ahadi ya kuunda upya utawala wake na kuzikonga nyonyo za wapiga kura waliokuwa na mashaka kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika 2022.

Macron anaiunda upya serikali yake wakati Ufaransa ikipambana na hali ya kudorora kwa uchumi tangu Vita vya Pili vya Dunia, kudidimia huko kutafanya uchumi ushuke kwa asilimia 11 mwaka 2020 na kurudisha nyuma mafanikio yaliopatikana baada ya bidii kubwa ya kutokomeza ukosefu wa ajira, limeripoti shirika la habari la Reuters.

Wawekezaji watakuwa wanaangalia kuona iwapo Waziri wa Fedha Bruno Le Maire, ambaye alisimamia mageuzi kuboresha uchumi na kutumia fedha nyingi kuyanusuru makampuni kama Air France na Renault kuendelea kuzalisha wakati wa mtikisiko wa kiuchumi, ataendelea na nafasi yake katika mabadiliko haya.

“Tukirejea kutoka mapumziko ya kipindi cha joto hali itakuwa ngumu, lazima tujitayarishe,” Macron ameyaambia magazeti ya eneo katika mahojiano yaliyochapishwa jioni Alhamisi.

Ofisi ya Macron imesema mrithi wa Philippe atatajwa saa kadhaa zijazo. Chanzo cha habari kinachofahamu jinsi Macron anavyofikiria kimesema rais hatamrejesha madarakani waziri mkuu, kama inavyotokea katika baadhi ya nyakati Ufaransa inapofanya mabadiliko ya serikali.