Prigozhin alionekana kwenye video – ambayo huenda ilirekodiwa barani Afrika - kwenye kurasa za mtandao wa Telegram zinazohusishwa na kundi la Wagner.
Prigozhin anaonekana amesimama katika eneo la jangwa akiwa amejificha na akiwa na bunduki mikononi mwake. Kwa mbali, kuna watu wengi wenye silaha na lori la mizigo.
Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha eneo hilo au tarehe ya video hiyo, lakini maoni ya Prigozhin na baadhi ya machapisho katika kurasa zinazounga mkono kundi la Wagner yaliashirira kwamba video hiyo ilirekodiwa barani Afrika.
"viwango vya Joto ni zaidi ya nyuzi 50. Kila kitu ni kama tunavyopenda. Kampuni ya Wagner inaifanya Russia kuwa kubwa zaidi katika mabara yote, na Afrika - huru zaidi. Haki na furaha - kwa watu wa Afrika, tunafanya maisha magumu kwa ISIS na Al- Qaeda na majambazi wengine," Prigozhin anasema kwenye video.
Kisha anasema Wagner inaajiri watu na kikundi hicho "kitatimiza kazi zake." Video hiyo pia inaambatana na nambari ya simu kwa wale wanaotaka kujiunga na kikundi.