Papa Francis awakosoa walio kiuka masharti ya kudhibiti COVID-19

Papa Francis akiongea baada ya maombi ya kila wiki katika maktaba kwenye maktaba ya Apostolic Palace, Disemba 30, 2020. (Credit: Vatican Media)

Papa Francis Jumapili amewakosoa watu walio safiri nje ya nchi kwa ajili ya sikukuu na kukiuka amri ya masharti dhidi ya virusi vya corona, akisema walitakiwa kuonyesha uelewa zaidi juu ya taabu wanazopata watu wengine kutokana COVID-19.

Akiongea baada ya maombi yake ya mchana ya kila wiki, Francis amesema alikuwa amesoma ripoti za magazeti juu ya watu kusafiri kwa ndege ili kukimbia katazo la serikali na kwenda kustarehe sehemu nyingine, shirika la habari la Reuters linaripoti.

“Wao hawakuwafikiria wale waliokaa majumbani, kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayo wakabili watu wengi walioathiriwa na amri ya kutotoka nje, na wagonjwa. (Walijifikiria wao wenyewe) tu na kwenda mapumzikoni na kufurahi,” Papa alieleza.

Papa Francis akifanya maombi kutoka katika maktaba ya Apostolic Library, Vatican.

“Hili kwa hakika lilinisikitisha sana,” alisema katika hotuba yake iliyorekodiwa katika video kutoka kwenye maktaba ya Apostolic Palace mjini Vatican.

Utamaduni wa maombi ya kuitakia dunia baraka kwa kawaida hufanyika wakati Papa akiwa kwenye roshani mkabala na uwanja wa Mtakatifu Peter, lakini yalihamishiwa ndani ili kuzuia mikusanyiko yoyote ya watu na kudhibiti kuenea kwa COVID-19.

“Hatujui kile kilichopangwa kwa ajili yetu katika mwaka 2021, lakini kile ambacho wote tunaweza kukifanya kwa pamoja ni kufanya bidii kidogo zaidi kusaidiana. Kuna majaribio ya kuangalia tu masilahi yetu binafsi,” ameongeza kusema.

Nchi nyingi zimeweka masharti makali kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, ambavyo vimewaua watu zaidi ya milioni 84 ulimwenguni, kwa mujibu wa hesabu za karibuni za shirika la habari la Reuters.