Papa Francis atuma salaam maalum za Krismas Sudan Kusini, Ulimwenguni

Papa Francis akiongoza ibada ya Krismas katika Kanisa la Mtakatifu Peter, Disemba 24, 2019, Vatican. (Photo by Alberto PIZZOLI / AFP)

Katika salamu zake za Sikukuu ya Krismas kwa jiji la Vatican na ulimwengu, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis alieleza hisia zake juu ya watu waliolazimishwa kuhama nchi zao kutokana na dhulma na watoto ambao wametelekezwa na wanakabiliana na madhila yanayotokana na uvunjifu wa amani.

Katika utamaduni wake wa kutuma ujumbe wa salamu na baraka za Krismas maarufu kama "Urbi et Orbi" kutoka katika dirisha la Kanisa la Mtakatifu Peter, papa amesema tafakuri zake zinaenda maeneo mengi ya duniani ambako kuna “kiza kutokana na sababu za kiuchumi, siasa za kieneo na ugomvi wa mazingira lakini alisema mwanga wa Kristo ni mkubwa zaidi.

Papa Francis alizungumza juu ya watoto wengi wanaoteseka kutokana na vita na migogoro iliyoko Mashariki ya Kati na akazitaja nchi za Syria, Lebanon na Iraq. Alizungumzia juu ya watu wa bara la Afrika, “ambapo hali ya kijamii na kisiasa mara nyingi imewasukuma watu kuhama nchi zao, na kuwanyima makazi yao na familia zao.

Alisema : “Ni kukosekana haki kunafanya wavuke majangwa na bahari ambayo yanakuwa makaburi yao. Ni dhulma ndiyo inapelekea kuingia katika mateso yasioelezeka, utumwa wa kila namna na mateso katika kambi zenye vizuizi.” Na papa ameongeza “Ni dhulma ambayo inayowafanya maeneo ambapo kungeweza kuwa na matumaini kuishi maisha ya ubindamu yenye heshima, lakini badala yake wanajikuta kwenye vizuizi.

Hivi leo papa pia ametuma wito maalum wa amani na mafanikio kwa viongozi wa Sudan Kusini. Ujumbe wa pamoja na wa salamu za Krismas Askofu wa Kanisa la Anglikan Justin Welby na Mchungaji John Chalmers. mratibu wa zamani wa Kanisa la Scotland, imewahakikishia viongozi wa Sudan Kusini ukaribu wao wa kiroho na viongozi hao wakati wakifanya juhudi ya kutekeleza mkataba wa amani uliofikiwa kwa ajili ya nchi yao.

Katika Ujumbe wa Krismas, Papa Francis pia alieleza tafakuri zake juu ya watu wa Venezuela, ambao wamezingirwa na migogoro yao ya kisiasa na kijamii, na Ukraine, inayotaka suluhisho thabiti litakalo leta amani ya kudumu.

Usiku wa Jumanne wakati wa kuanza kwa kilele cha ibada yasikukuu ya Krismas, kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulitangazwa kwa waumini waliohudhuria ibada hiyo.

Papa Francis alisema : “Baraka za Mungu, zinazoleta uokovu kwa wote, umeufunika ulimwengu usiku huu.” Pia alikuwa na ujumbe wa mapenzi yasiokuwa na shuruti. “Krismas inatukumbusha kuwa Mungu anaendelea kutupenda sote, hata wale waovu kuliko wote.

Papa alisema : “Wewe unaweza kuwa na fikra potofu, unaweza kuwa umevuruga mambo kabisa, lakini Bwana anaendelea kukupenda>”

Papa Francis atajitokeza tena kuwasalimu makundi ya watu katika Bustani ya Mtakatifu Peter Alhamisi na Jumapili na ataadhimisha maombi ya kumshukuru Mungu kwa kumalizika mwaka Disemba 31 katika kanisa la Mtakatifu Peter.