Papa Francis ametoa salamu za Krismasi, akiombea amani kwa dunia iliyoathirika na vita na vitisho vya ugaidi.
Alizungumza kutoka baraza la kanisa kuu la Saint Peter’s, mkuu wa kanisa la Kikatholiki alizungumza moja kwa moja na watu wanaotaabika kutokana na vita vya Syria, hasa katika mapigano ya kikatili ya mji wa Aleppo, na kuihimiza jumuia ya kimataifa kutafuta suluhisho la mzozo wa nchi hiyo kwa njia ya mazungumzo.
Akiwahutubia maelfu na maelfu ya waumini walokusanyika kwenye uwanja wa St Peter kuhudhuria hotuba yake ya mwaka ya 'Urbi et Orbi', Kwa Mji na Kwa Dunia, Papa Francis alisema ugaidi unapanda mbegu za hofu na vifo katika miji na nchi kote duniani.
Kwa upande wake mkuu wa kiroho wa kanisa la Uingereza Askofu wa Canterbury Justin Welby, wafuasi milioni 85 wakianglikana, alitoa ujumbe sawa na huo wa Papa akizungumzia wasiwasi ulotanda kote duniani.
Usalama kwa upande mwengine uliimarisha katika makanisa kote ulaya kukiwepo na onyo kwamba magaidi wakislamu huwenda wanapanga mashambulizi dhidi ya wakristo wanapoadhimisha siku kuu yao mashuhuri ya kidini.
Kwengineko kote duniani wachristo waliendelea na sherehe zao za kitamaduni kuadhmisha siku ya kuzaliwa Yesu Kristo.
Kwenye mji wa Bethlehem, kwenye Ukingo wa Magharibi, maelfu ya waumini walihudhuria misa katika Kanisa la Nativity, lililojengwa kwenye mahala alipozaliwa Kristo.
Nchini Irak mamia ya wakristo walihudhuria Ibada ya hadharani katika mji wao wa Bratella karibu na Mosul ikwa kama ni ishara ya matumaini na kukaidi vitisho vya magaidi.
Rais wa Marekani Barack Obama na familia yake walisherekea siku kuu hii mjini Hawaii, ambako wanapumzika.