Pakistan yachunguza mauaji ya vinyozi sita yaliyotekelezwa kwa kupigwa risasi

FILE - Mwanajeshi akilinda katika eneo la mpakani kati ya Afghanistan huko North Waziristan, Pakistan Oktoba 18, 2017.

Miili ya watu sita waliouawa kwa kupigwa risasi iligunduliwa mashambani huko North Waziristan, wilaya ya kikabila kaskazini magharibi mwa Pakistan katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa linalopakana na Afghanistan.

Marehemu hao walitambuliwa kuwa ni vinyozi kutoka jimbo la mashariki la Punjab, nchini Pakistan.

Akizungumza na idhaa ya Kiurdu ya VOA, Afisa wa Polisi wa Wilaya Roohan Zeb Khan alieleza kuwa tukio hilo la mauaji hayo ni la kigaidi.

Alisema kuwa mauaji hayo yanachunguzwa na miili hiyo itakabidhiwa kwa familia zao baada ya zoezi la kuwatambua kukamilika.

Haji Mujtaba, mwandishi wa habari katika eneo, alisema vinyozi wote walikuwa na maduka yao katika soko hilo hilo huko Mir Ali, mji mkubwa wa pili huko North Waziristan. Alisema watu hao walitekwa siku moja kabla ya tukio hilo.

Hakuna kundi lililodai kuhusika hadi sasa, lakini uwepo wa wanamgambo wenye silaha, hususan kutoka katika kundi lililopigwa marufuku la Tehreek-e-Taliban Pakistan, au TTP, umeongezeka kwa kiwango kikbuwa katika wilaya mbalimbali za kikabila tangu Taliban ya Afghanistan kurejea madarakani katika upande wa pili wa mpaka hapo Agosti 2021.

Taliban walipoingia madarakani mara ya kwanza nchini Afghanistan kuanzia 1996 hadi 2001, wanaume walipigwa marfuku kunyoa ndevu zao au kukata nywele kuwa fupi au mkato wa mitindo inayovuma. Wale walio kaidi mara nyingi waliadhibiwa kwa kupigwa, huku nywele zao zikinyolewa.

TTP iliweka masharti kama hayo kwa Wapakistani baada ya wanamgambo kuchukua udhibiti wa eneo la bonde la Swat mapema katika miaka ya 2000. Utawala wao wa vitisho ulimalizika baada ya operesheni yz kijeshi kufanyika mwaka 2009.

Vipeperushi viliwakataza vinyozi kuwakata nywele wanauma katika mtindo fulani ambavyo vilionekana katika maeneo ya kikabila ya Pakistan katika miezi kadhaa iliyopita.

Haiko bayana, hata hivyo, iwapo vinyozi sita hao walilengwa kwa kazi yao.

Katika taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari jioni, TTP imekanusha kuhusika na tukio hilo.

Ripoti ya Sarah Zaman wa VOA imechangiwa na Shamim Shahid wa idhaa ya Urdu ya VOA