Netanyahu alizungumza baada ya ripoti za vyombo vya habari vya Israel kusema kuwa maelewano yanafikiwa kati ya Washington na Tehran ambayo yangejaribu kurudisha nyuma mpango wa nyuklia wa Iran kwa kiasi fulani, badala ya kuondolewa kwa vikwazo.
Ripoti hizo hazikuweza kuthibitishwa moja kwa moja, na Marekani imekanusha hadharani mpango kama huo.
Maafisa wa Israeli wanaamini kuwa baadhi ya maelewano tayari yamefikiwa, ya kudhibiti urutubishaji, na kwamba baadhi ya fedha ambazo zilikuwa zimeshikiliwa, zimeachiliwa. Viongozi hao walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa sababu walikuwa wakijadili tathmini ya siri ya kidiplomasia.
Tovuti ya habari ya Israeli iitwayo Walla, wiki jana iliripoti kuwa chini ya maelewano yanayoibuka, Iran itapunguza urutubishaji wake wa uranium hadi asili mia 60, kwa sharti la kuondolewa vikwazo.
Tovuti hiyo pia ilisema pande zote mbili zinajadili uwezekano wa kubadilishana wafungwa.
Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Marekani ya Mambo ya Nje Matthew Miller alisema "hakuna mpango kama huo," na kuongeza kwamba ripoti hizo hazikuwa za kweli.