Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC ashutumu uzuiaji wa misaada kwenda Gaza

Moshi ukifuka kufuatia shambulio la anga la Israel huko Rafah, Oktoba 30 2023. Picha na SAID KHATIB / AFP.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Karim Khan alionya siku ya Jumapili kwamba kuzuiwa kwa misaada ya kibinadamu kuingia Gaza kunaweza kuwa uhalifu.

"Kuzuia misaada kama inavyoelezewa na maazimio ya Geneva kunaweza kupelekea uhalifu ndani ya mamlaka ya mahakama," Khan aliwaambia waandishi wa habari mjini Cairo.

Alikuwa akizungumza baada ya kutembelea kivuko cha Rafah nchini Misri, ambako alisema malori yaliyokuwa yamejaa bidhaa muhimu yamekwama na yanashindwa kuvuka kuingia Gaza.

"Niliona malori yaliyojaa bidhaa, yakiwa yamejaa misaada ya kibinadamu yamekwama mahali ambapo hakuna mtu anayeihitaji, yamekwama nchini Misri, yamekwama Rafah," alisema.

"Vifaa hivi lazima viwafikie raia wa Gaza bila kuchelewa."

Rafah ndio kituo pekee cha kuingilia, ambapo misaada ya kimataifa kwa sasa inaweza kupita na kuingia katika ardhi ya Palestina inayoshikiliwa na Hamas, ambayo imekuwa ikibabiliwa na kuzingirwa kabisa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel.

Israel ililizingira na kufanya kampeni yake kubwa ya mashambulizi ya mabomu baada ya watu wenye silaha wa Hamas kufanya uvamizi na kuvuka mpaka a tarehe 7 Oktoba, na kuua watu 1,400, wengi wao wakiwa raia, na kuwachukua mateka 230, kulingana na maafisa wa Israel.

Tangu wakati huo mashambulizi ya Israel yameua zaidi ya watu 8,000, nusu yao wakiwa watoto, wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas katika eneo hilo ilisema.

Misaada kidogo ilianza tena kupitia katika kivuko cha Rafah Oktoba 21, jumla ya malori 117 yameingia.

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP