Mkuu wa jeshi la Sudan afanya mazungumzo na rais wa Misri

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi (kulia) akimpokea kiongozi wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan huko El Alamein Agosti 29, 2023. Picha na Urais wa Misri / AFP.

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan amekuwa na mazungumzo na mshirika wake mkuu rais Abdel Fattah al Sisi siku ya Jumanne katika mji wa El Alamein kaskazini mwa Misri, ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuzuka kwa vita mwezi Aprili.

Jenerali al-Burhan aliondoka wakati, madaktari na mashuhuda wakisema raia 39 waliuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, katika shambulio la makombora katika mji wa Nyala katika jimbo la Darfur Kusini ambako mapigano kati ya jeshi na wanamgambo yamepamba moto.

Picha zilizochapishwa mitandaoni zilionyesha dazeni ya miili imefunikwa kwa sanda kando ya barabara, huku wanaume wakionekana wanawazika watu kwenye kaburi kubwa la pamoja.

Baraza tawala la kijeshi la Sudan SCS, linasema kiongozi huyo wa Sudan amekua na mazungumzo na rais al-Sisi kuhusu hali ya vita nchini mwake na juhudi za kujaribu kumaliza vita hivyo pamoja na masuala yanayohusiana na ushirikiano kati ya nchi zao mbili.

Misri imependekeza kua mpatanishi kati ya makundi yanayopigana huko Sudan, baada ya juhudi kadhaa za kimataifa za kujaribu kumaliza vita hivyo kushindikana.

Siku ya Jumatatu al-Burhan alitoa hotuba kali kwa wanajeshi wake alipowatembelea kwa mara ya kwanza katika mji wa Port Sudan, akiapa kupambana hadi kukomoesha uwasi anaodaiwa ulianzishwa na kikosi cha dharura cha RSF ambacho anakitaja kua ni cha mamluki.

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alipoitembelea kambi ya jeshi ya Flamingo iliyoko Port Sudan, Agosti 28, 2023. Picha na AFP.

"Tunakusanyika kila mahali ili kuushinda uasi huu, tushinde uhaini huu, na mamluki hawa wanaotoka maeneo mbalimbali ya dunia," alisema Burhan akishangiriwa na wanajeshi.

"Hakuna muda wa majadiliano kwa sasa. Tunaelekeza nguvu zetu zote kwenye vita, ili kukomesha uasi," alisema Burhan.

Matamshi yake yametolewa siku moja baada ya kiongozi wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Daglo kutoa taarifa inayoelezea vipengele kumi vya "muelekeo" wa kumaliza vita na kujenga "taifa jipya".

Vita kati ya Burhan na Daglo aliyekuwa makamu wake wa zamani aliyegeuka kuwa mhasimu wake mkubwa, vimekuwa vikiendelea tangu Aprili 15.

Vita hivyo vilianzia katika mji mkuu wa Khartoum na kuenea haraka hadi majimbo ya Darfur, Kordofan na Jazira, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni kuyakimbia makazi yao.

Kwa miezi kadhaa, kikosi cha RSF kimekua kimemzingira Burhan ndani ya makao makuu ya jeshi huko Khartoum, lakini wiki iliyopita jenerali huyo alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza na kuanza ziara ya kukagua majeshi katika sehemu kadha za nchi hiyo.