Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 17:54

Kenya: Duru mpya ya mazungumzo kati ya serikali na upinzani yameanza kutafuta suluhu


Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, akiwa na aliyekuwa Makamu wa Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakati akizindua ripoti maalum kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa ghasia zinazojirejea za uchaguzi Novemba 2019.
Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, akiwa na aliyekuwa Makamu wa Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakati akizindua ripoti maalum kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa ghasia zinazojirejea za uchaguzi Novemba 2019.

Duru mpya ya mazungumzo ya pande mbili kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kupitia wawakilishi wao kwa  lengo la kupata ufumbuzi juu ya kupanda kwa  gharama ya maisha na matokeo ya uchaguzi wa urais yameanza Jumatano.

Mazungumzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka, aliyekuwa mjumbe wa amani wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta nchini Sudan Kusini, anayeongoza ujumbe wa upinzani pamoja na Kimani Ichung’wah, kiongozi wa shughuli za serikali katika bunge la taifa ni kiongozi wa ujumbe wa serikali wamekubaliana kuwasilisha matakwa ya kila upande na kanuni za ushiriki.

Wamekubaliana pia kuwepo hadidu za rejea zitakazoelekeza asili na mkondo wa majadiliano kufikia Jumatatu wiki ijayo, kama hatua ya wazi ya kuzuia kuvunjika kwa majadiliano kama ilivyotokea katika duru ya kwanza.

Musyoka, amesema kuwa pande hizo mbili zimekubaliana kuweka mbele maslahi ya umma na kuahidi kujadiliana kwa nia njema kufikia matokeo ya haki kwa changamoto zinazolikabili taifa, kwa sasa na kwa siku zijazo.

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la Taifa Kimani Ichungwah, amesisitiza kuna haja kwa pande zote mbili kuingia kwenye mazungumzo yatakayofikia muafaka na kuliweka taifa kwenye mkondo wa ufanisi, kisiasa na kiuchumi.

Hadi sasa hakuna muda uliotolewa wa kumalizika kwa mazungumzo hayo. KIla upande unawakilishwa na wanachama watano kutoka kila upande.

Hili litakuwa jaribio la pili kwa mazungumzo ya pande mbili baada ya awali ya mwezi wa Mei kuvunjika baada ya upinzani kujiondoa.

Ruto na Odinga wameweka wazi kuwa mazungumzo haya hayatahusisha mfumo wa kugawana madaraka ila ni kusuluhisha matatizo ya Kenya ambapo kila raia wa taifa hilo atajihisi kuwa ni sehemu ya serikali, lakini Bw Odinga tayari ameonya kuwa upinzani utarejea mitaani mwezi Septemba iwapo hapatakuwa na maafikiano.

Mazungumzo haya yanafanyika kufuatia mkutano wa ana kwa ana kati ya Ruto na Odinga chini ya upatanishi wa rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, kujaribu kuwarai viongozi hawa kuweka kando tofauti zao na kuweka mbele maslahi ya taifa.

Wafuatiliaji wa siasa za Kenya, wanaeleza kuwa Ruto na Odinga katika shinikizo kuepuka kuvunjika kwa duru hii mpya ya mazungumzo, kama anavyosemamfuatiliaji wa siasa za Kenya Mark Bichache.

Kuelekea duru hii mpya, pande mbili zimekuwa zikikinzana hadharani kuhusu mambo yanayostahili kujadiliwa kwenye meza ya mazungumzo.

Serikali ya rais Ruto imesisitiza kuwa majadiliano haya yanastahili ikiwa ni hatua ya mazungumzo ya kuundwa upya kwa tume ya uchaguzi, kuanzishwa kwa hazina ya ustawi wa maeneo bunge, utekelezaji wa sheria ya theluthi mbili ya jinsia, kuundwa kwa ofisi rasmi ya kiongozi wa upinzani na kuhalalishwa kwa kwa ofisi ya mkuu wa mawaziri.

Lakini upinzani unasisitiza majadiliano ni sharti yahusu gharama ya juu ya maisha, ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022, mageuzi kwenye tume ya uchaguzi na mfumo wa kuzuia kuingiliwa kwa vyama vya kisiasa na mfumo wa uongozi wa taifa.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.

Forum

XS
SM
MD
LG