Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 11:19

Mabalozi waomba majadiliano kati ya Ruto na Odinga


Polisi wa Kenya wakirusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Picha na Luis Tato / AFP.
Polisi wa Kenya wakirusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Picha na Luis Tato / AFP.

Mabalozi wa nchi za Ulaya na Marekani wanasikitishwa na vifo, vurugu na uharibifu wa mali ikiwa ni pamoja na matumizi ya risasi kuwatawanya waandamaanaji wanaolalamikia dhidi ya hali ngumu ya maisha nchini Kenya.

Mabalozi hao kumi na tatu wakiongozwa na balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman, kupitia taarifa ya Jumanne kwa vyombo vya habari, siku moja kabla ya duru ya tatu kuanza ya maandamano yanayoipinga sheria ya fedha ya mwaka 2023, ya serikali ya rais Ruto, ambayo inasababisha ongezeko kubwa la ushuru kwa bidhaa muhimu, kupanda gharama za maisha pamoja na kutaka haki katika uchaguzi uliopita.

Wanadiplomasia hao kutoka Marekani, Uingereza, Ujerumani, Uholanzi, Uswidi, Uswisi, Ufini, Denmark, Ireland, Norway, Ukraine, Canada na Australia wanasikitishwa na idadi ya vifo na majeruhi yanayotokana na maandamano hayo na kuwataka rais Ruto na mpinzani wake mkuu Raila Odinga kufanya mazungumzo ili kuepusha vurugu, machafuko, ghasia pamoja na uharibifu wa mali.

Katika taarifa yao ya pamoja pia wanaeleza hali ya kutoridhishwa na matumizi ya risasi katika kuwatawanya waandamaanaji.

Aidha, wameonyesha kuwa wako tayari kuingilia na kukutanisha pande zote mbili mezani ili kufikia suluhu. Wamesema kuwa Ruto na Odinga wana wajibu wa kuhakikisha hakuna vifo zaidi au uharibifu wa mali.

Mbali na upinzani kuonyesha nia ya kushiriki katika mzungumzo na wanadiplomasia hao, Jumanne umezishtumu nchi za magharibi kwa kutofanya lolote kuhusu maafa yaliyotokea wakati wa maandamano.

Mfanyikazi akimwaga maji kwenye kizuizi kinachowaka huko Nairobi, Julai 12, 2023. Picha na Luis Tato / AFP.
Mfanyikazi akimwaga maji kwenye kizuizi kinachowaka huko Nairobi, Julai 12, 2023. Picha na Luis Tato / AFP.

Mbali na rais Ruto kupiga marufuku kufanyika kwa maandamano yoyote wiki hii, lakini upinzani umesisitiza kuwepo kwa maandamano na kutoa ratiba ya kufanyika kwa maandamano hayo kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.

Wamesema serikali imewaondolea walinzi vinara wa Muungano huo wakiwemo Odinga na Kalonzo Musyoka, Waziri Mkuu wa zamani na Makamu wa rais, mtawalia, ambao wote kwa mujibu wa katiba, serikali inastahili kuwapa ulinzi.

Shirika la kutetea haki za binaadabu la Human Rights Watch linasema kuwa serikali ya Kenya inapaswa kuepuka kuchukua hatua zinazoonekana kuharamisha haki ya kuandamana, ambayo inalindwa chini ya sheria za Kenya na sheria za kimataifa za haki za binadamu pamoja na kuacha kuwaita waandamanaji kuwa magaidi na kuheshimu haki za binadamu za kukusanyika na maandamana kwa amani.

Jumatano iliyopita, kwa duru ya pili katika kipindi cha wiki moja, wafuasi wa upinzani walizuia biashara katika miji mikubwa nchini Kenya huku polisi wakijikuta na wakati mgumu kuyatawanya makundi hayo ya waandamanaji kwa kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya kutoa machozi.

Katika ghasia zilizotokea wakati wa maandamano hayo, watu wasiopungua kumi wameripotiwa kuuawa baada ya kupigwa risasi katika miji ya Kisumu, Kajiado, Migori, Kisii, Makueni na Machakos na wengine kuheruhiwa, kulingana na taarifa ya serikali ghasia hizo zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali.

IMETAYARISHWA NA KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

Forum

XS
SM
MD
LG