Katika ujumbe kwa shirika la habari la AFP, mkuu wa mkoa wa Pwani Rhoda Onyancha anasema "Jumla ya vifo - 403, vimeorodheshwa sasa, kufuatia awamu ya hivi karibuni ya kufukua makaburi katika msitu wa Shakahola, ambako kiongozi wa dhehebu hilo Paul Nthenge Mackenzie anatuhumiwa kuwataka wafuasi kubaki na njaa mpaka kufa.
"Ufukuaji utaendelea kesho," Onyancha aliongeza, wakati wachunguzi wakitafuta makaburi zaidi katika msitu huo, ambapo walipatikana waathiriwa wa kwanza -- wengine wakiwa wamekufa, wengine wakiwa hai lakini wakiwa dhaifu na kuodhoofika -- walipogunduliwa tarehe 13 mwezi Aprili.
Kulingana na uchunguzi wa serikali kuhusiana na miili hiyo, njaa inaonekana kuwa chanzo kikubwa cha vifo, ingawa baadhi ya waathiriwa wakiwemo watoto walinyongwa, kupigwa au kuzibwa pumzi.
Mackenzie, dereva wa zamani wa teksi aliyegeuka kuwa mhubiri, amewekwa chini ya ulinzi wa polisi tangu katikati ya mwezi Aprili.
Tarehe 3 Julai, mahakama katika mji wa bandari wa Mombasa iliongeza muda wa kuzuiliwa kwake kwa mwezi mmoja wakisubiri uchunguzi ukamilike.
Waendesha mashtaka wa serikali wamesema Mackenzie anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi au mauaji ya halaiki, lakini bado hajatakiwa kukubali au kukana mashtaka dhidi yake.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.
Forum