Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:52

Ruto asema hatafumbia macho uhalifu


Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa jirani na majengo ya biashara zilizoteketeza moto wakati wa maandamano huko Kisumu Julai 12, 2023. Picha na REUTERS/James Keyi.
Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa jirani na majengo ya biashara zilizoteketeza moto wakati wa maandamano huko Kisumu Julai 12, 2023. Picha na REUTERS/James Keyi.

Serikali ya Kenya Alhamisi imesema takribani watu kumi wamefariki na zaidi ya 300 akiwemo mbunge mmoja wamekamatwa kufuatia maandamano yaliyoitishwa na mkuu wa upinzani Raila Odinga yakipinga serikali ya rais William Ruto

Maandamano hayo yaliyofanyika Jumatano ikiwa ni ya pili katika kipindi cha wiki moja yalizua ghasia na kusababisha hasara na kusitisha biashara katika miji mikubwa ambako maandano yamekuwa yakifanyika.

Waziri wa usalama Kindiki Kithure, amesema kwamba watu 312 ambao wanadaiwa kupanga, kuandaa au kufadhili maandamano yaliyopigwa marufuku na polisi wamekamatwa na watafunguliwa mashtaka akiwemo mbunge na kusisitiza kuwa msako unaendelea kuwakamata watu zaidi waliohusika na maandamano hayo inayoyamithilisha na ugaidi.

Maandamano hayo yanayopinga utawala wa Ruto pamoja na sheria mpya ya fedha ya mwaka 2023, na mzigo wa kodi kwa bidhaa za kimsingi na kupanda kwa gharama za maisha.

Polisi wakijikuta katika wakati mgumu wakitawanya makundi hayo ya waandamanaji kwa kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya kutoa machozi.

Kutokana na machafuko katika maandamano hayo, vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti watu kumi wameuawa baada ya kupigwa risasi katika miji ya Kisumu, Kajiado, Migori, Kisii, Makueni na Machakos na wengine kujeruhiwa.

Serikali ya rais Ruto pia inaeleza kuwa imepata hasara ya shilingi milioni mia saba, ambazo ni sawa na dola milioni tano za Kimarekani kutokana na uharibifu uliofanyika kwenye sehemu ya barabara kuu ya Nairobi Expressway yenye umbali wa kilomita 27.1, katika eneo la Mlolongo baada ya kufungwa vituo vya huduma za ushuru.

Watu wakibeba bidhaa kutoka katika majengo ya biashara zilizokuwa zikiteketea na moto huko Kisumu Julai 12, 2023. Picha na REUTERS/James Keyi.
Watu wakibeba bidhaa kutoka katika majengo ya biashara zilizokuwa zikiteketea na moto huko Kisumu Julai 12, 2023. Picha na REUTERS/James Keyi.

Ruto, Alhamisi, ameuonya upinzani kuwa hawezi kutishwa na matukio ya uharibifu wa mali ya umma, vurugu, ghasia na rabsha zinazoondoa utulivu wa nchi huku akimshtumu Raila Odinga kwa kuivuruga serikali yake. Mara kwa mara, rais Ruto amekuwa akiulaumu utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa matatizo ya kiuchumi ya Kenya.

Akizungumza na vyombo vya habari muda mfupi baada ya Ruto, Odinga ametangaza kuwa wiki ijayo upinzani utaandaa duru ya tatu ya maandamano.

Aidha, kiongozi huyo wa upinzani aliwalaumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na kusababisha maafa yaliotokea.

Mfuatiliaji wa masuala ya uchumi Charles Karisa, amesema kwa sasa uchumi wa Kenya hauwezi kustahimili vitisho zaidi baada ya kuathiriwa na janga la COVID na msukosuko wa kifedha duniani.

Maaskofu wa Kanisa Katoliki, Jumatano, wamemtaka Rais Ruto kufuta sheria ya fedha ya mwaka 2023 na serikali yake kukomesha ukopaji wa ndani ili kuwezesha benki kukopesha biashara za kibinafsi zinazoendesha uchumi wa ndani kama hatua ya haraka ya kuleta utulivu nchini humo. Maaskofu hao pia wamemkata rais Ruto kutekeleza sera na kuweka mikakati ahadi za matumaini alizowapa Wakenya.

IMETAYARISHWA NA KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

Forum

XS
SM
MD
LG