Wito wa kuwepo kwa Muungano wa Afrika (AU) yenye nguvu umepigiwa debe katika mkutano wa tano wa uratibu wa Mwaka wa Kati wa Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Nairobi.
Mkutano huo uliongozwa na Rais wa Kenya. William Ruto ambaye alitoa wito wa mageuzi ya AU yanayozingatia uhuru wa kifedha kwa Muungano huo.
Rais William Ruto amesema inawezekana kujenga Afrika iliyounganishwa zaidi, yenye ustawi na utulivu huku akiongeza kuwa ilikufanikiwa ni lazima iendeshwe na Afrika na watu wake, viongozi na rasilimali zake.
Aidha Rais Ruto alisema kuwa hatua ya kuanzia inapaswa kuwa mageuzi ya Umoja wa Afrika. Alisikitika kwamba zaidi ya miongo mitano baada ya uhuru, bara bado linategemea ufadhili kutoka nje kuendesha ajenda zake.
"Lazima tuachilie AU kutoka kwa vikwazo ili iweze kutekeleza hatua za dharura na muhimu katika bara hili kwa kutumia rasilimali zinazozalishwa ndani," alisema Rais Ruto”
Umoja wa Afrika (AU) walikutana chini ya kaulimbiu ya mwaka ya AU ya Kuharakisha Utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara katika Bara la Afrika. Kauli ambayo imekuwa ikipigiwa debe ilikutoa nafasi bora kwa mataifa ya Bara la Afrika kufanya Biashara kwa njia rahisi.
Ruto alikiambia kikao hicho kuwa ushirikiano wa Afrika hauwezi kuzuilika kwani utafungua milango ya mabadiliko ambayo hayajawahi kushuhudiwa.
Alisema eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika litakuwa eneo kubwa zaidi la biashara huria, likileta pamoja nchi 54.
"Soko hili moja litainua watu milioni 30 kutoka kwa umaskini uliokithiri na kuongeza mapato." ," alisema Amina”
Akihutubia kikao cha ufunguzi, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed alisema kuwa Afrika ndiyo chimbuko la suluhu la changamoto za dunia nzima.
Ulimwengu sasa unakabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa kutokana na milipuko ya coronavirus, mabadiliko ya hali ya hewa, na vita nchini Ukraine. Afrika inaelemewa na changamoto hizi, aliongeza.
“Mkutano huo unatoa fursa nzuri ya kutimiza matarajio ya watu wa Afrika na Ajenda ya 2063”
Amina aidha aliongeza kuwa nchi za Afrika zinaungwa mkono kikamilifu na Umoja wa Mataifa, akitolea mfano wito wa sekretarieti ya G-20 ya kuchukua hatua za kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
“Ni lazima tuwe na sauti dhabiti katika G-20 inayofafanua ubunifu na mawazo ya Afrika, na lazima pia tuwe na hatua za pamoja za viongozi wa Afrika”
Alisema mabadiliko ya hali ya hewa yameweka mizigo zaidi katika bara la Afrika, akitoa wito wa kustawisha ushirikiano miongoni mwa viongozi wa Afrika ili kutetea maslahi ya Afrika katika vikao vya kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema Utangamano unaouzungumzia unapaswa kujengwa kwa kuzingatia hali ya kisiasa na hali ya kiuchumi kama inavyotokea ulimwenguni kwa sababu Afrika inakabiliwa na matokeo ya utawala wa ulimwengu na athari za shida ya kifedha ambayo inaathiri bara la Afrika.
“Kwa kweli Afrika inapaswa kuja na msimamo wake wa pamoja wa afrika kushughulika na Biashara, uhamiaji, ufadhili wa maendeleo na utatuzi wa migogoro” Alisema Moussa Faki”
“Kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa tumeona madhara yake na Rais William Ruto kwa nafasi yake kama mwenyekiti wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi amekuwa mzuri katika kuendesha na kutetea maslahi ya amani na usalama wa Afrika na duniani kote”alisema Moussa Faki”
Mkutano huu ulihudhuriwa na viongozi wa Afrika akiwemo Rais wa Comoro Azali Assoumani, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais wa Djibouti Ismail Guelleh, Ali Bongo wa Gabon, Rais wa Nigeria Bola Tinubu Miongoni mwa wengine.
Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda, Taratibu za Kikanda na Nchi Wanachama wa AU zilihudhuria mkutano huo uliomalizika Jijini Nairobi.
Ripoti ya Hubbah Abdi wa VOA Swahili, Nairobi, Kenya
Forum