Miili zaidi imepatikana kutoka katika eneo la ajali ya ndege Nepal

Ndugu wa watu waliokuwemo katika ajali ya ndege wakihuzunika nje ya uwanja wa ndege huko mjini Pokhara, Nepal, Jumapili Mei 29, 2022.

Kundi la uokozi linalofanya msako katika maeneo ya milima huko Nepal Jumatatu wamepata miili ya watu 17 kati ya watu 22 waliokuwemo kwenye ndege iliyoanguka jana, maafisa wamesema.

Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la ndege la Tara Air msako bado unaendelea kujaribu kuwapata watu ambao inasemekana pengine wamekwama katika mabaki ya ndege.

Kundi la waokozi linafanya kazi kwa kutumia mikono yao bila kuwa na vifaa maalumu na imekuwa vigumu kusogeza mabaki ya chuma.

Ndege ya Tara Air Turboprop Twin Otter, ilipoteza mawasiliano na uwanja wa ndege siku ya Jumapili wakati ikisafiri kufuatana na ratiba kwa safari ya dakika 20 katika eneo la mto wenye kina kirefu na vilele vya milima.

Raia wanne wa India na wawili kutoka Ujerumani walikuwemo katika ndege hiyo , Tara Air imesema.

Wana hewa watatu na abiria wengine walikuwa ni raia wa Nepal. Mabaki hayo yaligunduliwa na wanakijiji ambao walikuwa katika eneo hilo ambalo hujulikana kama Himalaya Viagra, hiyo ni kulingana na taarifa za kieneo.