Ndege inayomilikiwa na shirika la ndege la Eastern, nchini China, iliyokuwa imebeba watu 132 imeanguka kusini mwa China, katika sehemu ya milimani.
Shirika la habari la serikali limeripoti kwamba ajali hiyo imewaka moto baada ya kuanguka, lakini hakuna taarifa kamili kuhusu vifo wala majeruhi.
Mamlaka ya safari za ndege nchini China imesema kwamba ndege hiyo aina ya Boeing 737, iliyokuwa inasafiri kutoka mji wa Kunming, ikielekea mji wa Guangzhou, ilipoteza mawasiliano ikiwa katika anga ya mji wa Wuzhou.
Ilikuwa imebebea abiria 123 na wafanyakazi wa ndani ya ndege 9.
Shirika la habari la serikali CCTV, limeripoti kwamba maafisa wa uokoaji wanaendelea na shughuli ya uokoaji.
Mara ya mwisho kuripotiwa ajali ya ndege nchini China ilikuwa mwaka 2010, ambapo ndege ya shirika la Henan ilianguka kaskazini mwa mkoa wa Heilongjiang, na kuua watu 42.
Ajali mbaya zaidi ya ndege kutokea China ilikuwa mwaka 1994 ambapo watu 160 waliuawa.