Katika dhifa ya chakula cha jion siku ya Jumanne, Charles alielezea "masikitiko makubwa" kwa vile alivyoviita vitendo vya unyanyasaji vya kuchukiza na visivyofaa vilivyofanywa dhidi ya Wakenya wakati wa mapambano ya uhuru.
Rais William Ruto alipongeza hatua ya mwanzo ya mfalme huyo yakwenda nje ya "hatua za majaribio na za usawa za miaka iliyopita," lakini alisema mengi yanahitaji kufanyiwa kazi.
Mfalme Charles III alikutana na wanajeshi wakongwe wa Kenya waliopigana katika vita vya pili vya dunia siku ya Jumatano, baada ya kukiri kwamba "hakuna kisingizio" kwa manyanyaso yaliyofanywa na utawala wa Uingereza wakati wa enzi ya ukoloni katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Charles alisema alitamani "kuongeza uelewa wangu kuhusu makosa haya" wakati wa ziara yake ya siku nne nchini Kenya akiwa na Malkia Camilla, lakini pia kuimarisha "ushirikiano wa kisasa wa usawa unaokabili changamoto za leo".
Katika siku ya kwanza ya ziara yake mjini Nairobi Jumanne, mkuu huyo wa taifa la Uingereza mwenye umri wa miaka 74 alisema "makosa ya siku za nyuma yanasababisha huzuni na masikitiko makubwa", lakini hakuomba msamaha.
"Kulikuwa na vitendo vya kuchukiza na visivyofaa vya unyanyasaji vilivyofanywa dhidi ya Wakenya walipokuwa katika ... mapambano ya kudai uhuru na mamlaka. Kwa hilo, hakuna kisingizio," alisema katika hafla ya kitaifa.
Siku ya Jumatano, Charles na Camilla walitembelea makaburi huko Nairobi, kuwaenzi Waafrika waliopoteza maisha kwa ajili ya Uingereza katika vita viwili vya dunia, wakiweka shada la maua mbele ya makaburi yao kabla ya kukutana na wanajeshi wakongwe wa Kenya, wengine wakiwa kwenye viti vya magurudumu.
"Natumai tunaweza kufanya kitu maalum kwa ajili yenu," Charles alimwambia mmoja wa maveterani wakati akiwakabidhi medali wanajeshi wa zamani, sehemu ya mpango wa Uingereza kutambua kwa kuchelewa mchango wa vikosi visivyo vya Ulaya katika juhudi za kivita.
Uingereza ilikubali maelewano ya nje ya mahakama na kulipa fidia ya dola milioni 24 mwaka 2013 kwa zaidi ya waathirika 5,200 walionyanyaswa wakati wa uasi wa Mau Mau, lakini ilikataa kuomba msamaha na kukanusha madai ya jamii nyingine.
Balozi wa Uingereza nchini Kenya, Neil Wigan, alikiambia kituo cha redio cha nchi hiyo wiki iliyopita kwamba msamaha ungeipeleka nchi yake katika "eneo ngumu la kisheria."