Mdahalo huo uliokuwa na malumbano makali ulifanyika katika mji wa wakulima wa Magharibikati, jimbo la Iowa, ambalo linafanya mkutano wa kwanza wa uteuzi wa mgombea urais chini ya wiki moja.
Malumbano na Tuhuma
DeSantis na Haley walitumia muda wote wa saa mbili wa mdahalo huo kulumbana na kuchukua muda mchache kumkosoa mgombea anayeongoza katika kinyang’anyiro hicho, Rais wa zamani Donald Trump.
Alipoulizwa iwapo anadhani Trump ana hadhi ya kuongoza nchi, Haley alijizuia kujibu swali hilo moja kwa moja, akisema rais ajaye anahitaji “kuwa na maadili.”
Gavana huyo wa zamani wa South Carolina alikuwa thabiti kuhusu matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020, ambao Trump amekuwa akikanusha, amesema “Trump alishindwa, [Rais wa Marekani Joe]Biden alishinda.”
'Aina ya Fikra ya Umoja wa Mataifa'
Katika moja ya masuala muhimu yaliyojitokeza, DeSantis alieleza uungaji mkono wa Haley katika kuidhinisha fedha kuwasaidia wananchi wa Ukraine akisema ni aina ya fikra ya Umoja wa Mataifa,” na kuangalia kama Marekani ina fedha zisizo na kikomo, akisema, “unaweza kumuondoa balozi kutoka Umoja wa Mataifa lakini huwezi kuiondoa Umoja wa Mataifa katika fikra ya balozi.”
Kuhusu mgogoro kati ya Israel na Hamas, DeSantis alisema “ Hamas wanataka kuwepo mauaji ya pili ya kimbari na hivyo Marekani lazima iiunge mkono Israel.” Haley pia anaiunga mkono Israel. DeSantis alisema haungi mkono suluhisho la kuwepo mataifa mawili ya Israel na Palestina.
Mashambulizi kufanyika Iran?
Hakuna mgombea atakaye unga mkono mashambulizi kufanyika ndani ya Iran kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa vita baina ya Israel na Hamas, lakini Haley “ anataka mifumo inayoiwezesha Iran kushambulia majeshi ya Marekani huko Iraq na Syria iondolewe.
DeSantis amezungumzia umuhimu wa kutenganisha uchumi wa China na Marekani, hususan katika uzalishaji wa dawa na silaha, kwa kuyapa makampuni ya Marekani motisha wa misamaha ya kodi na usimamizi.
Hakuna kuruhusu wahamiaji
Kuhusu wahamiaji wasiokuwa na makaratasi, Haley anaunga mkono kutotoa ruzuku kwa miji inayopokea wahamiaji, kuongeza wafanyakazi zaidi ya 25,000 wa udhibiti wa mipaka na mawakala wa ICE, na kubadilisha msemo “catch and release (kamata na kuachia) na kuwa “catch and deport” (kamata na kuwasafirisha).
Wakati wa mdahalo huo uliochukua saa mbili, DeSantis alimshambulia Haley kwa kubadilisha msimamo katika masuala muhimu, na kusababisha Haley kurejea mara kwa mara kuwaelekeza waliohudhuria mdahalo huo kwenda katika tovuti ambayo imeorodhesha kile anachokiita ni uongo wa DeSantis.
Ripoti ya mwandishi wa VOA Carolyn Presutti