Mawakili waomba mashtaka ya mauaji dhidi ya Kabuga yaondolewe

Felicien Kabuga

Mawakili wanaomwakilisha mshukiwa wa ufadhili wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, wameomba mashtaka dhidi yake yaondolewe, kwa madai kuwa hayuko katika hali nzuri kiafya kuweza kuendelea na kesi hiyo. 

Félicien Kabuga, mwenye umri wa miaka 84, alikamatwa mwaka mmoja uliopita nchini Ufaransa, na anazuiliwa mjini The Hague, Uholanzi, akisubiri kesi kuendeshwa katika mahakama, iliyo nchini Tanzania, inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kulingana na nyaraka za mahakama zilizoonekana na shirika la habari la Ufaransa, AFP, wakili wa Kabuga anasema kuendelea na kesi hiyo kwa sasa, ikizingatiwa hali yake ya kiafya ni ukiukaji mkubwa wa haki zake.

Kabuga, ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mmoja wa watu tajiri sana nchini Rwanda, anashutumiwa kwamba, kupitia kituo chake cha redio, alisaidia kuunda kundi la waasi wa Kihutu la Interahamwe, walioua idadi kubwa ya watu.