Mshukiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Félicien Kabuga anazuiliwa katika mahakama ya kimtaifa ya uhalifu – ICC, mjini Hague, baada ya kusafirishwa kutoka Ufaransa kufuatia amri ya mahakama ya Umoja wa Mataifa.
Kabuga, ambaye amekuwa mafichoni kwa zaidi ya miaka 22 hadi alipokamatwa nchini Ufaransa mwezi May, atafikishwa mbele ya mahakama ya ICC.
Wiki iliyopita, jaji katika mahakama ya Umoja wa Mataifa aliamuru kwamba Kabuga ahamishiwe Uholanzi, badala ya kuzuiliwa nchini Tanzania na mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia maswala ya afya kutokana na janga la virusi vya Corona.
Kabuga, mwenye umri wa miaka 84, anaweza kukaa ICC kwa miezi kadhaa na baadaye kesi dhidi yake kusikilizwa nchini Tanzania.
Waendesha mashtaka wa Umoja wa Mataifa wanamshutumu Kabuga, ambaye alikuwa mkulima mkubwa wa majani chai na kahawa, kwa kupanga mauaji dhidi ya maelfu ya watutsi na baadhi ya wahutu nchini Rwanda mwaka 1994 katika mashambulizi yaliyodhumu kwa muda wa siku 100.
Kabuga anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya halaiki ya watu, kuchangia mauaji hayo na uhalifu dhidi ya binadamu.
Amekana mashtaka dhidi yake akisema ni ya uongo.
Kwingineko, waendesha mashataka wa Uholanzi wamesema kwamba wamemkamata mwanamme raia wa Rwanda mwenye umri wa miaka 71 ambaye amekuwa akiishi Uholanzi kwa muda wa miaka 20, baada ya kupata ombi kutoka kwa serikali ya Kigali, la kutaka akamatwe na kurudishwa nchini humo.
Jina la mwanamme huyo halijatajwa lakini waendesha mashtaka wamesema mwanamme huyo alikuwa akifanya kazi katika benki na anamiliki duka la kuuza dawa, anayetuhumiwa kwa kuandaa orodha ya watutsi waliopangiwa kuuawa katika mashambulizi hayo yam waka 1994.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC