Tume ya uchaguzi ilianza kuhesabu zaidi ya kura milioni 600, katika uchaguzi uliochukua muda wa wiki sita, ukiwa ndio uchaguzi mkubwa zaidi kote duniani.
Matokeo ya mapema yanaonyesha kwamba chama chake Modi, cha Bharatiya Janata, kinaongoza kwa viti 280 kati ya 545 katika bunge la chini, kikiwa kimepata idadi kubwa ya viti zaidi ya idadi inayohitajika ya viti 272 kupata ushindi.
Chama cha upinzani cha Congress, kimepata viti 50.
Baadhi ya wafuasi wake Modi wanasema atasalia kuwa Waziri Mkuu muda wa kuwa yuko hai, wakimuombea kuwa na maisha marefu.
Modi alikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa chama cha Congress na kiongozi wake Rahul Gandhi, akikosolewa kwa usimamizi mbaya wa uchumi wa India pamoja na mapato madogo kwa wakulima kutokana na bei ndogo ya mavuno ya wakulima.
Lakini kampeni yake Modi ilipata kuungwa mkono kutokana na jinsi alivyojibu shambulizi la bomu la kutegwa kwenye gari, mwezi Februari, lililoua Zaidi ya maafisa wa usalama wa India 40 katika eneo lenye mzozo la Kashmir.
Ndege za kijeshi za India, zilivuka mpaka na kuingia katika nchi jirani ya Pakisan na kutekeleza mashambulizi dhidi ya kambi iliyodaiwa kuwa ya kutoa mafunzi kwa kundi la wanamgambo la Jaish-e-Mohammad, lililoripotiwa kuhusika na shambulizi la bomu la Kashmir.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.