Uamuzi huo wa kuwaruhusu wanawake kuingia ndani ya hekalu unakaidi katazo la mila ya Wahindu ya kupiga marufuku wanawake kuingia katika eneo hilo.
Takriban waandamanaji 400, wakiwemo wanawake wameandamana kwenye barabara za Kochi, katika mji wenye shughuli nyingi za kibiashara wa Kerala, wakiongozwa na chama cha Waziri Mkuu Narendra Modi cha Bharatiya Janata – BJP na kile cha Rashtriya Swaya-msevak Sangh -RSS), chama kikongwe kabla ya BJP.
Maduka yamefungwa, na shughuli za usafiri kusitishwa, madereva wakieleza hofu ya kushambuliwa iwapo wangebeba abiria.
Mahakama ya juu ya India, mwezi septemba, ilifutilia mbali marufuku ya kutowaruhusu wanawake waliobalekhe kuingia katika hekalu la mlima Sabarimala, ambalo huvutia mamilioni ya waumini kila mwaka.